Jiji la Dar es Salaam limerejea kwenye utulivu huku
shughuli za kibiashara na kijamii zikipamba moto, baada ya kipindi kifupi cha
mvutano kufuatia uchaguzi. Hata hivyo, athari za vurugu hizo bado ni kumbukumbu
chungu kwa wafanyabiashara wengi, ambao wanashukuru kurudi kwa amani na
kusisitiza umuhimu wa kulinda urithi huo wa kitaifa.
Mfanyabiashara Mzee Elia Moshi Afunguka Mmoja wa
wafanyabiashara wakongwe, Elia Moshi, ametoa ushuhuda wake wa kile
kilichotokea, akibainisha kuwa vurugu za hivi karibuni zilimwacha na majonzi
makubwa.
"Uchumi wa wengi ni mdogo, wanategemea kutoka
ndio wapate kula. Kilichotokea sitakisahau, kwani katika umri wangu huu mkubwa
sijawahi kukiona Tanzania," alisema Moshi.
Moshi alisisitiza kuwa matukio hayo hayakuwa
maandamano halisi, bali yalikuwa ni uvunjaji wa sheria uliotekelezwa na makundi
ya wahalifu.
"Yale hayakuwa maandamano, yalikuwa ni uvunjaji
wa sheria kwa kuharibu na kupora mali za watu binafsi na zile za umma.
Maandamano yanajulikana, watu hueleza hasira zao kwa kupitia maneno, lakini sio
vile. Makundi ya waporaji yalihusika na kuvunja amani," aliongeza kwa
msisitizo.
Kama Bw. Moshi, wafanyabiashara wengi wameathirika
moja kwa moja na machafuko hayo, hasa wale wanaotegemea kipato cha kila siku.
Maandamano na vurugu za muda mfupi ziliwarudisha
nyuma wafanyabiashara wengi kibiashara, hasa wale wadogo ambao hutegemea mtaji
mdogo na mzunguko wa haraka.
Baada ya kurejea kwa amani, wafanyabiashara sasa
wanatoa wito wa "Kazi na Utu," wakisisitiza kuwa biashara ziendelee
tu na kwamba ni muhimu "Maisha yaendelee sasa."
Kwa pamoja, wananchi wa Dar es Salaam wanakubaliana
kwamba amani ni msingi wa maisha na maendeleo yao, na haipaswi kuchezewa.

0 Maoni