Taifa la Tanzania linaonekana kuibuka na somo kubwa
kufuatia kipindi kifupi cha machafuko na vurugu, huku wananchi wengi
wakisisitiza tena na tena umuhimu wa amani, mazungumzo, na umoja kama njia
pekee ya kusonga mbele. Kauli ya "Kataa Uchochezi" imekuwa wito wa
kitaifa baada ya athari za vurugu za hivi karibuni kuonekana wazi.
Kutokana na maoni mengi ya wananchi kwenye majukwaa
mbalimbali, kuna hisia kali kwamba Watanzania wamekuja kutambua thamani halisi
ya amani baada ya kuipoteza kwa muda mfupi.
"Daaa kweli tumakuja kujua umuhimu wa amani
pale tulipoipoteza kwa muda," alisema mmoja wa wananchi Abdallah Mawata
akielezea hali hiyo. Mwingine aliongeza kwa msisitizo, "Tumeiona thamani
ya amani yetu."
Maoni haya yanawakilisha makubaliano mapana kwamba
machafuko na maandamano hayajengi, bali yanarudisha nyuma maendeleo ya taifa na
kuvuruga maisha ya kila siku.
Baraka Nyange mwendesha bodaboda alisema kwamba
kutulia kwa hali kunafungua milango ya shughuli za kiuchumi, jambo ambalo
wananchi wengi wanalikumbatia kwa mikono miwili.
Ingawa wananchi wameanza kufungua tena biashara zao,
kuendelea na kazi za mikono, na kurejesha utaratibu wa kulea familia katika
hali ya utulivu. bado tegemeo la kutoka kila siku kutafuta kipato cha
kesho,limeonesha umuhimu wa amani katika kulea familia.
Wananchi wameonyesha wasiwasi wao juu ya uharibifu
wa mali na miundombinu, wakisisitiza kuwa vitendo hivyo "vinakwamisha
maendeleo ya nchi yetu" na "vinarudisha nyuma sana uchumi." huku
wakisema kwamba hayakuwa maandamano bali uharibifu kwa kuwa maandamano mtu
anaeleza asichokipenda lakini si kwa kuifanya uharibifu na kupora.
Ujumbe mkuu unaojitokeza ni wito wa kulinda amani na
kukataa vitendo vyovyote vya uchochezi vinavyoweza kuvuruga utulivu wa taifa.
"Watanzania tuliende amani ya nchi yetu
tusikubali wapotoshaji wanao chochea kuvuruga amani ya nchi yetu," ni
kauli inayotolewa na wengi.
Ujumbe wa
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulisisitiza umuhimu wa mazungumzo,
mshikamano, na upendo kama njia bora ya kutatua tofauti.
Taifa sasa linaonekana kusimama kama taifa
lililojifunza, likisisitiza kwamba "Amani si udhaifu, ni nguvu
inayotuwezesha kusonga mbele," na kwamba Tanzania bila vurugu na
maandamano inawezekana.

0 Maoni