Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) limesema linafuatilia kwa karibu na limepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania wenzetu, wakiwamo wanahabari
na wengine waliojeruhiwa.
TEF imesema
siku ya tukio la vurugu za Oktoba 29 ilipokea taarifa za vifo vya vijana na
askari polisi. Pia baadhi ya wananchi waliwasiliana na wahariri, kuomba msaada
wa kuulizia walipo ndugu zao.
Taarifa ya
TEF iliyotolewa na Mwenyekiti Deodatus
Balile imetoa pole kwa Watanzania waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika
vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, katika
kilichoanza kama maandamano ya amani, lakini kuishia kwenye uchomaji wa magari,
vituo vya mafuta, nyumba, kadhia zingine za kiafya kwa waliopiga kura na
hatimaye mauaji ya raia na askari.
TEF imesema
inawakumbuka kwa heshima wanahabari na Watanzania waliouawa katika vurugu hizi,
kwani wameacha pengo kubwa katika tasnia ya habari, kazini na familia zao. Pia imewapa
pole wote waliojeruhiwa katika matukio hayo.
Jukwaa limesema
limerejea utamaduni wa Taifa letu wa amani na utulivu na kuakisi yaliyotokea
yakazaa maafa haya. Tunafahamu yapo maumivu makubwa kila upande, ila tunaomba
sasa tusimame pamoja kama taifa, tuzungumze na kujisahihisha, ili kamwe haya
yasitokee tena katika ardhi ya Tanzania, imesema taarifa hiyo.
Jukwaa limetoa
wito kwa Mamlaka kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka.
TEF imeisihi
Serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano haraka, ili kuponya majeraha kwa
pande zote.
Tunaomba
kila upande mchakato ukianza uwe tayari kushiriki kama nchi tumalize kadhia hii
milele, TEF imesema.
TEF
imemalizia taarifa hiyo kwa kusema tumeshuhudia madhara ya amani kupotea na
tulikofika, tujizuie kama nchi isitokee tena. Mungu awape uponyaji wa haraka
walioumia, azilaze mahali pema peponi roho za waliopoteza uhai, na atupe nguvu ya
kusimama kama nchi tujisahihishe. Mungu ibariki Tanzania.

0 Maoni