Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya
Kilwa Kisiwani na Songo Mnara wilayani Kilwa imeendelea kuwa kivutio kikubwa
kwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo tarehe 31 Oktoba 2025 ilipokea
jumla ya watalii 147 kutoka mataifa mbalimbali duniani waliowasili hifadhini
humo kwa kutumia meli ya kifahari iitwayo SH Diana, kwa lengo la kutalii na
kujionea vivutio vya kihistoria vilivyopo katika eneo hilo.
Watalii hao walitoka katika nchi 13 zikiwemo Ufaransa,
Australia, Ubelgiji, Canada, Uingereza, Uswisi, Ujerumani, Cyprus, New Zealand,
Marekani, Urusi, Uturuki na Ukraine. Ziara hiyo iliratibiwa na kampuni za
Savannah Tours Ltd kwa kushirikiana na Black Willow Safaris.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya watalii hao, Kamanda wa
Hifadhi hiyo, Mhifadhi Mwandamizi Kelvin Stanslaus, alisema ujio wa wageni hao
ni ishara njema kwa ukuaji wa utalii wa urithi nchini, hasa ikizingatiwa
umuhimu wa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kama maeneo yaliyosajiliwa na UNESCO
kuwa Urithi wa Dunia tangu mwaka 1981.
“Tunayo furaha kubwa
kuona wageni kutoka pande mbalimbali za dunia wakija kujionea historia adhimu
ya Kilwa, ambayo ni alama muhimu ya biashara ya kimataifa ya karne za kati kati
ya Afrika Mashariki na Dunia,” alisema Afisa huyo.
Aidha, wageni hao walipata fursa ya kutembelea majengo ya
kihistoria ikiwemo Msikiti Mkongwe, na
Kasri la Sultani, ambapo walivutiwa na usanifu wa majengo ya mawe pamoja na
simulizi za kihistoria zinazoambatana na maeneo hayo kutoka Kwa Maofisa wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA waliobobea na kutopea
katika masuala ya malikale.
Kwa mujibu wa TAWA ambayo ndiyo wasimamizi wa hifadhi hiyo, ujio wa meli hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuimarisha utalii wa urithi, hususan katika maeneo ya bahari, malikale na visiwa vyenye thamani ya kihistoria.



0 Maoni