WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ahakikishe wafugaji wote walioingiza
mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu wa mazao na
wananchi kukosa chakula wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwani hakuna yeyote
aliye juu ya sheria wananchi wote ni sawa.
“Serikali iko macho na
itamchukulia hatua yeyote anayeathiri shughuli za wengine, Tanzania ni nchi
inayoendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, hivyo watendaji wote wa
vijiji wawajibike kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuepusha migogoro
isiyokuwa na tija. Tutaendelea kuwalinda wananchi. Ukifuata utaratibu hakuna
shida, tufuate sheria.”
Ametoa agizo hilo jana
wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Namkatila, Matambarale na
Nandandala akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa
wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Vijiji hivyo ni miongoni mwa maeneo
yaliyoathirika zaidi na migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo mkulima mmoja
aliuawa.
Mheshimiwa Majaliwa
ameongeza kuwa Serikali haitovumilia kuona jamii ya wafugaji wasiozingatia
sheria na haitotoa nafasi kwa wakulima kuendelea kuharibiwa mazao yao. “Jambo
hili halikubaliki na hatua kali zitachukuliwa kwa watu wote wanaotaka kuvuruga
amani, Serikali haitovumilia vitendo hivyo.”
“…Hatutamsamehe mfugaji
anayetumia fimbo yake kumpiga mkulima baada ya kulisha mifugo kwenye shamba
lake. Hatuna nafasi ya kushuhudia hayo, utaratibu lazima uzingatiwe, lazima
tukomeshe migogoro ya wafugaji na wakulima. Tumuache mkulima aendelee kulima
avune. Tusilinde waovu.”
Waziri Mkuu amesema kwamba
kauli ya Serikali ya kuthamini shughuli za kilimo na ufugaji nchini haimaanishi
kuwa wafugaji wanaruhusiwa kuingiza mifugo na kulisha kwenye mashamba ya
wakulima, wala wakulima kudhuru mifugo ya wafugaji hivyo amewasisitiza wafanye
shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu kwani tayari serikali
imeshaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya makazi,
huduma za kijamii, kilimo na mifugo hivyo hakuna mwenye haki ya kumvamia
mwingine.
Amesema watendaji wa vijiji
wahakikishe kabla ya kuwakaribisha wafugaji katika maeneo yao wajiridhishe kama
wana maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo na pia wawashirikishe
wanakijiji husika juu ya ujio wa wafugaji na wafahamu idadi ya mifugo
waliyonayo. “Wananchi tulieni mkiona maeneo yenu yamevamiwa toeni taarifa. Hapa
tusisikie tena athari hizi.”
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za
kilimo na wasiogopewa kwani Serikali ipo makini na inaendelea kuimarisha ulinzi
katika maeneo yote nchini vikiwemo na vijiji vyao. Wananchi hao walimuelezwa
kuwa wanaogopa kuendelea na maandalizi ya mashamba kutokana na kuhofia uvamizi
wa mifugo.
Katika hatua nyingine,
Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesisitiza
kuwa wananchi lazima wafikishiwe huduma mbalimbali za kijamii karibu na makazi
yao, hivyo kwa kushirikiana na watendaji wengine wa Serikali atahakikisha
miradi yote ya maendeleo inasimiwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwemo kukamilika
kwa wakati na kwa viwango kusudiwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
baada ya wananchi wa kijiji cha Namilema kumuomba awasaidie kukamilisha ujenzi
wa zahanati ya kijiji hicho iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi ambao
wamekamilisha ujenzi wa boma. Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe zahanati hiyo
inakamilika.
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni