Bodi na Menejimenti ya MSCL watakiwa kusimamia kikamilifu miradi ya serikali

 

Bodi na Menejimenti ya Huduma za Meli nchini (MSCL) wametakiwa kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na serikali ili kuhakikisha fedha iliyotolewa kwa ujenzi inaleta thamani.

Maagizo hayo yametolewa Jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ukarabati wa meli tatu zitakazogharimu shilingi bilioni 48.092 pamoja na uzidunzi wa meli ya Mv Umoja iliyogharimu shilingi bilioni 21.

Naibu Waziri Kihenzile amesema kusainiwa kwa miradi hiyo mitatu kunalenga kukidhi mahitaji ya usafiri kwa abiria hususani katika Ziwa Tanganyika na kutumia fursa zilizopo katika kuhudumia masoko ya nchi jirani.

"Ukarabati wa meli ya kubeba abiria na mizigo ya MV Liembe itasaidia kurejesha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo, meli MT Nyangumi itasaidia usafirishaji wa shehena ya mafuta kuelekea nchi ya Uganda na Sudan ya Kusini, pamoja na Meli ya MT Ukerewe itakuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya shughuli za uokozi katika ziwa Victoria wakati wa dharura," amesema Kihenzile.

Amefafanua kuwa ukarabati wa meli hizo utawasaidia wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika pamoja na nchi za jirani za DRC, Burundi na Zambia, hivyo na serikali imeweza kuonesha kuwa wameanza kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla ameeleza kuwa usafiri wa njia ya maji ni tegemeo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na ni kichocheo kikubwa kwa wananchi wa ukanda huo katika kukuza uchumi.

Makilagi amefafanua kuwa ujio wa meli hiyo ya MV Umoja itakuwa ni chachu kwa Watanzania pamoja na kuleta matokeo chanya yenye tija katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mwanza na ukanda wa ziwa Victoria na Taifa kwa ujumla.

"Hii inatokana na usafiri wa meli kuwa na bei rahisi ya usafiri ukilinganisha na usafiri mwingine wote ni mashahidi kwa wale tunaosafiri," amesema Makilagi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Meli (MSCL) Eric Hamis amesema meli ya MV Umoja kabla ya ukarabati ilikuwa inabeba mabehewa 19 na baada ya ukarabati inauwezo wa kubeba mabehewa 22 na tani 1200 ya mizigo.

"Meli hii tayari imeanza kutoa huduma kati ya Mwanza na Bandari za Uganda na hivyo kufungua usafirishaji wa shehena ya mizigokupitia ushiroba wa kati kuelekea Nchini Uganda na Sudan ya kusini," alisema Hamis.

Meli ya kubeba mizigo ya MV Umoja inayobeba shehena ya mizigo katika Ziwa Victoria imefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu kiasi cha dola za Marekani 8,422,840 ambazo ni sawa na sh, 19,811,446,192 za Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni