TASAC yaanika fursa lukuki sekta ya usafirishaji majini

 

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nelson Mlali, amebainisha kuwapo kwa fursa nyingi katika sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji, ambazo Watanzania wanapaswa kuzichangamkia.

Bw. Mlali ametoa kauli hiyo jana Jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Ametaja miongoni mwa fursa hizo kuwa ni pamoja na kuanzisha usajili wa meli kwa masharti rafiki, uanzishwaji wa maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika Ukanda wa Pwani.

Maeneio mengine ni uanzishwaji wa maegesho ya boti ndogo katika Ukanda wa Pwani, uanzishwaji wa viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki, ujenzi wa bandari rasmi za uvuvi zenye tija kwa nchi na nchi jirani ili kukuza mapato.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Mlali amesema, utendaji kazi kwa umakini wa hali ya juu wa shirika hilo, umewezesha kupata hati safi mfululizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.

Kuhusu miradi amesema, TASAC wanaendelea na miradi mitatu ambayo ni mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria, unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024, ujenzi wa boti tano za uokozi (Ziwa Victoria 2, Tanganyika 2 na Ziwa Nyasa 1) na uendelezaji na uimarishaji wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA.

Pia amesema shirika linakabiliana na changamoto ya mabadiliko ya haraka ya teknolojia katika sekta na mahitaji makubwa ya mifumo ya TEHAMA pamoja na uhaba wa wataalamu wa ndani katika baadhi ya taaluma hasa wakaguzi wa usalama wa vyombo vya usafiri majini.

TASAC ilianzishwa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 53 lilitolewa tarehe 16 Februari, 2018.

Chapisha Maoni

0 Maoni