Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wadau
wa Sekta ya Madini imeanza maandalizi ya kushiriki Maonesho Makubwa ya Madini
Barani Afrika ya Mining Indaba.
Maonesho hayo yatakayofanyika mwezi Februari 2024, katika
jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini yatashirikisha wafanyabiashara, watoa
huduma, taasisi mbalimbali za kisekta pamoja na wakuu wa kampuni kubwa za
uchimbaji madini duniani.
Akizungumza wakati akiwasilisha mpango wa ushiriki wa
Tanzania katika Maonesho hayo kwa Waziri wa Madini kwa niaba ya Sekretarieti ya
maandalizi, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Mhandisi Philbert Rweyemamu amesema
ni moja ya maonesho ambayo huwakutanisha wawekezaji wapatao angalau 900,
taasisi za sekta zipatazo angalau 40 na watendaji wa kampuni wapato 1000.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Madini Mhe.
Anthony Mavunde amesema ushiriki watanzania Katika Maonesho hayo unatarajia
kuiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika na dunia nzima huku ukileta sauti moja
kwa wadau kuielewa Tanzania.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri
Mahimbali amesema dhamira ya Wizara ni kuweka ushiriki wa pamoja katika banda
moja la wizara, taasisi na wadau ili kufanya ushiriki wenye tija zaidi kwa
Tanzania.
Tanzania inatarajia kutumia maonesho ya Mining Indaba
kuvutia mitaji, uwekezaji, kujifunza, kuleta teknolojia bora za uchimbaji,
kujenga mahusiano ya kibiashara, kuimarisha ushirikiano pamoja na mambo
mengine.
Kampuni zinazotarajia kudhamini ushiriki wa Tanzania katika
maonesho hayo ni pamoja na Anglo Gold Ashanti, Barrick Gold, Shanta Gold,
Mantra Tanzania, Tembo Nickel, TRX Gold, Petra Diamond na City Engineering Ltd.
#TanzaniaItakuwepo#
#MiningIndaba2024#
VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri
0 Maoni