Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki
amekabidhi cheti cha shukrani kwa wadhamini wa maonesho ya Saba ya Kimataifa ya
Swahili International Tourism Expo - S!TE kwa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) na kutambua
mchango wake katika kudhamini na kuwa
sehemu ya mafanikio ya maonesho hayo ambayo yalifana kwa kiwango kikubwa.
TAWA ni miongoni mwa mashirika na Taasisi za Serikali
zilizojitokeza kushiriki na kudhamini maonesho haya ya Kimataifa ya Utalii
yaliyofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 6 - 8 Oktoba,
2023 ambapo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda,
cheti hicho kimepokelewa na Mhifadhi Mwandamizi - Utalii Steven Madenge
Akifunga rasmi maonesho hayo kwa mwaka 2023, Waziri Kairuki
amewashukuru wote waliohudhuria na kushiriki katika maonesho haya lakini
kipekee amewashukuru TAWA kwa kuwapeleka Wanyamapori hai katika maonesho hayo
ambao kwa kiasi kikubwa wamechagiza na kuleta vionjo vya aina yake na ladha ya
kipekee katika maonesho hayo
"Niwashukuru kwa mara nyingine tena wote kwa kuhushuria
katika maonesho haya muhimu kwa Taifa letu lakini vilevile katika sekta hii ya
utalii, katika biashara ya utalii na uwekezaji wa utalii," amesema waziri
Kairuki.
"Niwashukuru pia TAWA kwa kuleta Wanyamapori hai
naamini kwa walioweza kutembelea mabanda hayo ya TAWA wameweza kufurahia
bustani ya Wanyamapori hao," ameongeza Mhe. Kairuki
Aidha, Waziri Kairuki amewakaribisha tena wadau wote katika
S!TE 2024 inayotarajiwa kufanyika tarehe 11 - 13 Oktoba 2024.
Na. Beatus Maganja- Dar es Salaam
0 Maoni