REKODI MPYA: Watalii wa ndani zaidi ya 700 wafurika - Tarangire

 

Rekodi mpya imeandikwa  katika Hifadhi ya Taifa Tarangire iliyopo mkoani Manyara baada ya kupokea watalii wa ndani zaidi ya 700 waliotembelea hifadhi hiyo inayosifika Tanzania kwa kuwa na makundi makubwa ya Tembo.

Watalii hao wa ndani waliotoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), wameingia leo tarehe 26.10.2023 wakiwa katika magari (Cruzer - Warbus) 108 yaliyokuwa yakiongozana mithili ya msafara wa Mfalme akiingia katika Kasri yake.

Umuhimu wa idadi hii ya watalii wa ndani, hautainufaisha Hifadhi ya Taifa Tarangire tu, bali itaongeza mzunguko wa fedha katika vijiji vya Minjingu, Kakoi na Olevolosi kwa manunuzi ya mahitaji muhimu watakayofanya wakati wa ziara hiyo.

Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Ndg. Joel Kamunyoge aliyeongoza kundi la watalii hao alisema kuwa ujio wao umetokana na wito uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kuwataka Watanzania kuvipenda, kuvithamini na kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania.

"Sisi TUGHE ni desturi yetu kila tunapomaliza vikao vyetu vya kila mwaka, kutembelea maeneo yanayochangia uchumi kwa taifa na katika ziara hii tumeona ni vyema kuungana na Rais wetu Dkt. Samia kutangaza utalii wa ndani na kuchangia pato la taifa kwa viingilio tulivyotoa."

Naye, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Hery Mkunda, amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kuboresha miundombinu ya barabara na sehemu za mapumziko zinazotumika kwa ajili ya kupata chakula "Picnic sites."

"Sikutarajia kwa idadi yetu hii, kama tungeweza kutalii kwa uhuru na bila msongamano, lakini tumeshangaa kuona barabara nyingi na nzuri zilizotuwezesha kuona wanyama wengi na kwa ukaribu zaidi", aliongeza Mkunda.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Beatrice Kessy, alisema kuwa hifadhi hiyo leo imeweka rekodi mpya ya kupokea idadi kubwa zaidi ya watalii wa ndani tangu kuanzishwa kwake 1970. "Idadi hii inatupa matumaini kama shirika kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vyetu."

"Tunawapongeza sana watanzania wenzetu kutoka TUGHE kwa kuona umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii nchini, pia kwa kuichagua Hifadhi ya Taifa Tarangire  kwa mwaka huu, hivyo ni rai yetu kama shirika kuwaomba watanzania wengine kuiga mfano wa TUGHE," aliongeza Kamishna huyo.

Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Tanzanite Corporate Limited Elina Benson Mwangomo, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuleta vikao Arusha, kwani imekuwa ni fursa kwake na timu yake kupata watalii hao.

"Vikao hivi vimekuwa ni fursa kwetu vijana kujipatia kipato kwa kuwatembeza watalii hawa katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, pia kikubwa zaidi nawashukuru TANAPA kwa sababu haikuwa rahisi kwa kampuni peke yetu kuongoza magari haya 108 na watalii waliokuwemo bila msaada wao,"  aliongeza Bi. Mwangomo.

Mbali na kundi hilo la watalii 750 kutoka TUGHE, hifadhi hiyo pia imepokea watalii wengine wa ndani 100 kutoka TASAF na 40 wa kampuni ya UNAFRICATE.

Na. Jacob Kasiri - Tarangire

Chapisha Maoni

0 Maoni