Rais Samia kuanza ziara ya nchini India kesho

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kesho anaanza ziara ya kitaifa ya siku nne nchini India kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya India Mhe. Droupadi Murmu, ziara ambayo itamalizika Oktoba 11, 2023.

Ziara hiyo inalengo la kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na India, hususan katika sekta za kimkakati za afya, viwanda na biashara, ulinzi na usalama, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji na kilimo.

Pia ziara hiyo ya Rais Samia nchini India inalengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kutoka nchi ya India.

Nchi ya India ni mdau mkubwa wa maendeleo Tanzania ambapo hadi sasa taifa hilo la bara la Asia linachukua nafasi ya tano kwa kiwango cha uwekezaji nchini Tanzania.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na India ulianza tangu mwaka 1961, ambapo India ilifungua ubalozi wake Tanzania mwaka 1961 na Tanzania nayo kufungua ubalozi wake India mwaka 1962.

Mwaka huu Tanzania na India zinatimiza miaka 62 ya mwendelezo wa urafiki na ushirikiano katika masuala mbalimbali.

Chapisha Maoni

0 Maoni