WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.
“Moja kati ya hatua hizo, ni kuziblacklist kwa sababu
makampuni hayo yapo, tutumie makampuni ambayo yana uaminifu badala ya kutumia
makampuni ambayo yanatuzalishia migogoro,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo kwenye kikao alichokiitisha
ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam,
Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi
iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.
“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi
wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni
mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni
miradi yao,” alisema Majaliwa.
Aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi
wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu
ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili
kuepusha mianya ya rushwa.
Pia aligiza watafutwe na kukamatwa vibarua ambao wanatembea
na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji. “Bw.
Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo
vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za
Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda
wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama.”
“Hawa ni vibarua, lakini wana ramani na wanavijua viwanja
vyote. Wao wanachofanya ni kufanya mauzo halafu wanapeleka kwa watu wao pale
Jiji na hati zinatoka. Kwa hiyo, watafutwe na wanyang’anywe zile nyaraka ili
wasiendelee kuuza viwanja,” aliagiza Majaliwa.
0 Maoni