Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amewataka
Watendaji wa Wizara na Taasisi kujipanga kimkakati kwa kubuni miradi yenye tija
kwenye Sekta ya Madini itakayowezesha kuongeza Bajeti ya Wizara na kuhakikisha
inakwenda sambamba na Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Dira ya
2030 Madini ni Maisha na Utajiri pamoja na Vipaumbele vya Taifa.
Ametoa rai hiyo wakati wa kikao chake na baadhi ya Watendaji
hao wa Wizara na Wakuu wa Taasisi za Wizara, ambacho pia kimehusisha watendaji
wanaohusika na masuala ya Mipango, Fedha na Rasilimaliwatu kilicholenga
kujadili na kujipanga kutekeleza maelekezo, vipaumbele vya Wizara, majukumu,
mipango na program mbalimbali ambazo zilijadiliwa wakati wa vikao vya Waziri wa
Madini Mhe. Anthony Mavunde alivyofanya na taasisi zote chini ya Wizara baada
ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini kwa lengo la kufahamiana,
kujengeana uelewa na kuweka mikakati ili kuongeza tija kwenye Sekta ya Madini
Aidha, katika kikao hicho, watendaji hao wamepata wasaa wa kufahamishwa
kuhusu namna ya kuandaa mipango na miradi ya kisekta yenye tija kwa taifa kwa
kuhakikisha inakwenda sambamba na vipaumbele vilivyopangwa na Wizara na vile
vya kitaifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi Mwandamizi kutoka
Tume ya Taifa ya Mipango Khalid Shekimweli amesisitiza kuwa miradi na mipango
inayopangwa na sekta ni vema ikazingatia maeneo makuu ya msingi ambayo ni
pamoja na kuzingatia masuala yanayohusu huduma muhimu za kijamii, yanayokusudia
kuondoa umaskini pamoja na kukuza uchumi.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Bw.
Augustino Olal ameeleza kuwa katika Mwaka wa Fedha wizara imepangiwa bajeti ya
Shilingi Bilioni 89.3 ambayo imelenga kutekeleza vipaumbele Sita vya Wizara na
kuvitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuongeza Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la
Taifa; kuendeleza Madini Muhimu na
Madini Mkakati; Kuwaendeleza na kusogezaHuduma za Ugani kwa Wachimbaji wadogo;
kuhamasisha shughuli za Uongezaji thamani Madini na kuhamasisha uwekezaji na Biashara katika sekta ya Madini
na Uanzishwaji wa Minada na Maoneshi ya Madini ya Vito.
0 Maoni