WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema usimamizi makini wa
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
umewezesha Taifa kuvuka malengo ya kupambana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI
(VVU)ya 95-95-95 yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2025.
“Leo hii tayari asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi
ya VVU wanajua hali zao, asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya
ARV na kati yao, asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye
damu. Jukumu kubwa la Taifa tulilonalo
ni kulinda na kuyaendeleza mafanikio haya kwa nguvu za pamoja na umoja hadi
tufikie malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030,” alisema Majaliwa.
Majaliwa ameyasema hayo jana alipomuwakilisha Rais Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa Juu ya Kuimarisha Ubia
Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa Uendelevu wa Mafanikio ya Mwitikio wa
UKIMWI nchini uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji
na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha kwa ajili ya afua mbalimbali
za UKIMWI ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust
Fund) na mipango mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla ili
malengo ya kutokomeza ugonjwa huo yaweze kufikiwa.
Akizungumzia kuhusu majumuisho yaliyotokana na mdahalo huo,
Waziri Mkuu amewahakikishia wadau na Watanzania wote kuwa Serikali imesikia na
kupokea yote yaliyotajwa katika mdahalo huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la
Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) na itayafanyia kazi. “Suala la ubia halikwepeki
tunatambua umuhimu wa ushirikiano na tutalitekeleza kwa maslahi mapana ya
Watanzania.”
“Licha ya hayo, Serikali itazidi kuimarisha ushirikiano na
wadau mbalimbali waliopo nchini na nje ya nchi hasa katika uwekezaji, kutoa
elimu, vifaa tiba, wataalamu, maboresho ya Sera na miongozo mbalimbali ya
masuala ya UKIMWI.Tumewasikia wadau na pia tumepata maoni kutoka kwa ndugu zetu
WAVIU. Maoni haya yatasaidia kuboresha mikakati ya Serikali katika kuhakikisha
tunafikia malengo,” alisema Majaliwa.
Amesema licha ya tafiti kuonesha kupungua kwa unyanyapaa na
ubaguzi dhidi ya VVU nchini, bado matendo ya unyanyapaa na ubaguzi na ukatili
wa kijinsia yanaendelea kuwa kikwazo katika kuzifikia na kuzitumia huduma za
VVU hasa kwenye jamii, Shuleni, vyuoni na mahala pa kazi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amempongeza
Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kupambana na masuala ya UKIMWI nchini.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kutokana na juhudi zako, maelekezo na uamuzi wa kuwa
Balozi wa kuhamasisha Wanaume kupima maambukizi ya VVU, uelewa kwa Watanzania
wanaofahamu hali zao kuhusu VVU umeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2016/2017
hadi kufikia asilimia 97 mwaka 2023.”
Naye, Mwenyekiti wa NACOPHA, Leticia Moris amesema baraza
hilo limetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, hivyo ameishukuru Serikali na
wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuhakikisha huduma mbalimbali zikiwemo dawa za
kufubaza VVU zinaendelea kupatikana.
0 Maoni