WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko aendelee kushughulikia suala la changamoto
ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.
“Watanzania wapate hii huduma, upatikanaji huu ni muhimu
kuhusisha taasisi zote za mafuta na wanunuaji mafuta kwa pamoja ‘bulk’ wakae
pamoja na Wizara zinazohusika ikiwemo Wizara ya Fedha na Idara ya Ofisi ya
Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu waone namna ya upatikanaji wa mafuta,” alisema
Majaliwa.
Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Septemba 7, 2023) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi katika kipindi cha maswali
kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni upi
mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta ya kutosha.
“Lakini pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta
mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Na kama hili litafanyika ndani ya wiki
moja tutakuwa tumeshapata majibu na kuwapa taarifa Watanzania.Tutahakikisha
nishati hii ya mafuta inapatikana na Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo,”
alisema Majaliwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI
iendelee na utaratibu wa kubaini maboma yote kwenye sekta ya afya na elimu
ambayo waliyajenga na hayakukamilika, wahakikishe wanaendelea kutenga fedha kwa
ajili ya kuyakamilisha kwa sababu yametokana na bajeti zao.
Waziri Mkuu amesema suala la ujenzi wa miradi ya elimu au
afya ambayo inahusisha majengo ni mkakati ulioelekezwa katika Mamlaka ya
Serikali za Mitaa kupitia fedha zinazopelekwa kutoka Serikali Kuu ambazo
zinapelekwa kujenga majengo hayo kwa thamani ya jengo kutokana na makadirio
waliyoyatoa, hivyo wanatakiwa wasimame ujenzi ukamilike kama ilivyokusudiwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema chanzo kingine ni fedha
inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri zenyewe ambapo wao hupanga
mipango ya maendeo yao kupitia bajeti yao na kwenda kujenga, maboma mengi
yanatokana na mipango yao, hivyo wayakamilishe.
“Uzoefu tulioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hii, majengo
ambayo yametekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu yamekwenda kama yalivyo na
pale ambapo hayakukamilika hatua kali zimechukuliwa. Sasa kwa kuwa maboma mengi
yanatokana na mipango yao na kushindwa kuyaendeleza, mkakati wa Serikali ni
kuhakikisha maboma yote yanakamilika, “alisema Majaliwa.
Ametumia fursa hiyo kuziagiza zifanye tathmini ya miradi
yake ione maeneo gani ambayo walianza miradi na wameshindwa kukamilisha na
yamebaki maboma ili wapange bajeti ya kila mwaka kuhakikisha maboma hayo yanakamilika.
“Halmashauri haziwezi kushindwa kupata shilingi milioni 50 kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi wa zahanati”.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalum, Hawa Mwaifunga aliyetaka kujua ni nini mpango wa Serikali katika
kuhakikisha inakamilisha maboma ya kutolea huduma za elimu na afya nchini,
miradi iliyoanzishwa na Serikali na nguvu za wananchi ili wananchi hao waweze
kuona thamani ya nguvu yao na ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo
yao.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni