Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amevikumbusha
vyama vya siasa nchini kuwa Serikali ya awamu ya sita imeruhusu vyama vya siasa
kufanya mikutano ya hadhara kwa nia ya vyama hivyo vizungumzie sera zao,
mipango yao ili vyama vikue na virudishe wanachama waliopoteza.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam,
alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa
Demokrasia, na kuvisihi vyama vya siasa kutumia fursa hiyo kwa kunzigatia sheria
za nchi, mila na desturi zetu.
“Tumeruhusu mikutano ili vyama vikue na virudishe wale
waliowapoteza, hatukutoa fursa ili watu wakavunje sheria, watu wakasimame
kutukana, watu wakasimame kukashifu, watu wakasimame kuchambua dini za watu, “alisema
Rais Samia na kuongeza “Lakini sishangai kwanini haya yanatokea kwa sababu
yakuzungumzwa hakuna, hakuna…hakuna tulianza ooh na Katiba tukaenda ikakatika katikati,
bandari imeenda sasa Katiba tena, hakuna unapokuwa hakuna cha kusema utalazimisha
kunzungumza yasiyokuwepo”.
Rais Samia ameviomba vyama vya siasa nchini kwenda kutumia
fursa ya mikutano ya hadhara kujijenga kwa wananchi, waelezee sera zao, kuelezea
watafanya vipi na wamejipanga vipi ili wananchi warudi wawaunge mkono na watakapo
ingia kwenye uchaguzi vyama vyote viwe vimesimama vizuri.
Kuhusu Katiba mpya, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa
kutouteka mchakato wa Katiba mpya na kuwaeleza wazi kwamba Katiba si mali ya
wanasiasa bali ni mali ya Watanzania wote hivyo matengenezo yake yanahitaji
kazi kubwa.
“Viongozi wa kisiasa tunadhani kwamba tunayo haki ya
kuburuza watu tunachotaka kwenye Katiba ndio kitakua, hapana Katiba ni ya
Watanzania na inahitaji kueleweka na kila mtu ili iwe rahisi kutekelezeka kwa
vitendo,” alisema Rais Samia.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha Katiba mpya, viongozi wa
siasa watatoa maoni yao kwa Kamati itakayoanzisha mchakato wa Katiba mpa, na
watakuwa na wawakilishi wao lakini si kila mtu atakuwepo kwenye Kamati hiyo.
Mkutano huo wa siku tatu, wenye kauli mbiu ya "
Imarisha Demokrasia, Tunza Amani", umeitishwa na Msajili wa Vyama vya
Siasa kwa ajili ya kuyafanyia tathimini ya mambo yaliyoinishwa na Kikosi Kazi
cha Rais kilichoratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa
nchini.
0 Maoni