NIC Insurance yajivunia miaka mitatu ya mafanikio makubwa

 

Shirika la Bima la Taifa (NIC), limefanikiwa kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 76.45 2019/20 hadi kufikia shilingi bilioni 103.94 2021/22, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.98 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye, wakati akielezea mafanikio ya NIC Insurance katika mkutano wake na vyombo vya habari, ambapo amesema mafanikio hayo yametokana na hatua mbalimbali za mabadiliko zilizochukuliwa.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu NIC Insurance wamelipa madai ya bima za wateja ambapo hadi kufikia Juni 2022, wamelipa jumla ya shilingi bilioni 33.79 kwa bima za maisha na shilingi bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.

“Tumeweza kulipa kodi ya mapato Serikalini kutokana na faida inayopatinana ambapo ulipaji huo umeongezeka kutoka shilingi billioni 11.86 mwaka 2019/20 hadi shilingi bilioni 15.14 mwaka 2021/22 sawa na wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye

Ameongeza kwamba faida ya ghafi ya NIC Insurance imeongezeka kutoka shilingi bilioni 33.65 mwaka 2019/20 hadi shilingi bilioni 63.21 mwaka 2021/22 sawa na asilimia 43.91 kwa mwaka.

Aidha, amesema kutokana na faida mfululizo wameweza kupata malimbikizo ya faida ya shilingi bilioni 45.74 kufikia Juni, 2022 kutoka kiasi cha malimbikizo ya hasara ya shilingi bilioni 19.31.

Kuhusu mali za NIC Insuance amesema zimekua kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kutoka mali zenye thamani ya shilingi bilioni 350.36 mwaka 2019/20 hadi kufikia mali zenye thamani ya shilingi bilioni 423.99 mwaka 2022.Ukuaji huu ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10.51 kwa mwaka.

“Ufanisi katika uendeshaji, umewezesha ukuaji wa mtaji wa wanahisa kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 72.16 mwaka 2019/20 hadi Shilingi bilioni 217.07 mwaka 2021/22. Ukuaji huu wa mtaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 100.40 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.

Kwa upande wa uwekezaji Dkt. Doriye amesema uwekezaji katika hati fungani za Serikali kwa mwaka 2021/22 umefikia kiasi cha shilingi bilioni 105.64 ukilinganisha na kiasi cha shilingi bilioni 51.58 kilichokuwepo mwaka 2019/20. Ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 52.40 kwa mwaka.

Pia, uwekezaji katika amana za Benki mwaka 2021/22 umefikia kiasi cha shilingi bilioni 32.23 ukilinganisha na shilingi bilioni 19.53 kilichokuwepo mwaka 2019/20. Ongezeko hili la uwekezaji kwenye amana za Benki ni sawa na wastani wa asilimia 32.54 kwa mwaka.

Dkt. Doriye amesema kwamba usimamizi madhubuti wa matumizi pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kumeongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo na tija jambo lililoshusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida.

Kati ya makampuni zaidi ya 30 yaliyopo kwenye soko la bima Tanzania, NIC insurance imeweza kumudu ushindani huu kwa kufanya vizuri baada ya maboresho mbalimbali yaliyofanyika tangu mwaka 2019.

NIC Insurance ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa 100%, ikiwa na dhamana ya kufanya biashara ya bima za mali na ajali pamoja na bima za maisha. 

Chapisha Maoni

0 Maoni