Kamati ya Bunge yaitaka NHC kutilia mkazo ukusanyaji madeni

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linatilia mkazo ukusanyaji madeni ya wapangaji katika nyumba zake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Timetheo Mnzava amesema, pamoja na shirika hilo kujitahidi katika ukusanyaji malimbikizo ya kodi za wapangaji wake lakini bado linatakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni kutoka kwa wadaiwa.

Akizungumza wakati wa Kikao cha kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dodoma tarehe 25 Oktoba 2023, Mhe. Mnzava amelitaka pia shirika hilo kuweka msisitizo zaidi katika kuzuia kuzalisha madeni badala ya kusubiri mpaka wapangaji kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii wametaka kuwepo mikakati madhubuti itakayowaogopesha wapangaji ili waweze kulipa kodi zao kwa wakati.

Vile vile, Kamati hiyo imeonesha kuridhishwa na utendaji kazi wa shirika hilo katika kutekeleza miradi yake ambapo wamelitaka Shirika kuangalia namna ya kujenga nyumba za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi.

‘’Niipongeze NHC pamoja na Wizara ya Ardhi maana kazi za shirika zinaonekana hata kwa macho ila nisisitize muweke jitihada pia katika ukarabati wa nyumba zenu ili wapangaji wakae vizuri,’’ alisema mjumbe wa kamati Cecilia Paresso.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza mbele ya Kamati hiyo amesema, kwa sasa upo uhitaji mkubwa wa nyumba na serikali iko katika marekebisho ya sera ili kuwezesha ushiriki wa taasisi na sekta binafsi katika uzalishaji nyumba.

‘’Kama serikali tutahakikisha kasi ya ujenzi wa nyumba inaongezeka maana takwimu za sensa ya watu na makazi zimeonesha uhitaji mkubwa wa nyumba na uzalishaji ukiwa mdogo hivyo msisitizo ni kuzalisha nyumba za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi,’’ alisema Dkt. Mabula.

Na. Munir Shemweta- WANMM

Chapisha Maoni

0 Maoni