Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna
wa Polisi Benedict Wakulyamba amesisitiza nidhamu katika kutekeleza majukumu ya
kila siku na uadilifu katika kutunza na kulinda rasilimali za maliasili.
Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo Agosti 19, 2023, wakati
akiongea na watumishi wa TAWA- Kanda ya Kati sambamba na kukagua miradi
iliyotekelezwa kwa kupitia fedha za Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na
Mapambano dhidi ya UVIKO -19 katika Mapori ya Akiba Swagaswaga na Mkungunero
yanayopatikana katika Mikoa ya Dodoma na Manyara.
" Sisi ni Jeshi la Uhifadhi, na moja ya sifa ya msingi
wa Jeshi lolote duniani ni kusimamia mambo makubwa mawili ambayo ni uadilifu na
nidhamu," amesema Kamishna Wakulyamba.
Akizungumzia suala la uwepo wa wanyama wakali na waharibifu,
Kamishna Wakulyamba amesema jukumu letu sisi kama wahifadhi ni kuendelea
kudhibiti wanyamapori hawa ili wasilete madhara zaidi.
"Tuendelee kuweka mikakati madhubuti na tufanye kila
linalowezekana kuhakikisha kuwa tunawadhibiti wanyamapori wakali na
waharibifu," Sisi ni Jeshi! Jeshi halishindwi. Tutimize wajibu wetu.
" Lakini nitumie nafasi hii kumshukuru kwa dhati kabisa
Rais wetu kwa kuamua kuikuza sekta ya Utalii nchini na kuipatia Wizara ya
Malisili na Utalii kiasi cha Shilingi bilioni 90 kupitia Mpango wa Ustawi wa
Jamii na Mapambano dhidi ya UVIKO 10 ambapo TAWA ilipatiwa takriban bilioni
12.9 na leo tunashuhudia miundombinu ya kisasa ambayo imejengwa kupitia fedha
hizo," aliongeza Kamishna Wakulyamba.
Aidha, Kamishna Wakulyamba alieleza kuridhishwa na
utekelezaji wa miradi ya UVIKO 19 na kuipongeza Menejimenti ya TAWA kwa
usimamizi mzuri wa miradi hiyo. Vilevile alielekeza Menejimenti kutangaza
vivutio na fursa za uwekezaji vilivyopo katika Mapori hapo ili kuvutia wageni
na wawekezaji wengi katika maeneo hayo.
Awali, akitoa salamu za ukaribisho kwa niaba ya Kamishna wa
Uhifadhi -TAWA, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage
Kabange alimshukuru Kamishna Wakulyamba kwa ujio wake na kumhakikishua kuwa
maelekezo aliyoyatoa yatafika kwa watumishi wengine wa TAWA na hayataishia kwa
watumishi wa Kanda ya kati pekee.
Kwa upande wake, Kamanda wa Uhifadhi, Kanda ya Kati,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Herman Nyanda alieleza kuwa jumla ya miradi Mitano
imetekelezwa kupitia fedha za UVIKO -19 katika Mapori ya Akiba matatu
yanayopatikana Kanda ya Kati ambapo katika Pori la Akiba Swagaswaga limejengwa
lango la kisasa la kuingia wageni.
Kwa upande wa Pori la Akiba Mkungunero miradi iliyotekelezwa
ni ujenzi wa geti la utalii, barabara yenye urefu wa kilometa 52 na eneo la
kupumzika wageni (picnic site).
0 Maoni