Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Bw. Mobhare Matinyi amemtaka Mkandarasi anayejenga Soko la kisasa la Mbagala Zakhem
kuhakikisha anakamilisha na kukabidhi kabla ya Agosti 15 mwaka huu.
Bw. Matinyi ametoa maagizo hayo akizungumza mara baada ya kutembelea na kujionea maendeleo
ya ujenzi wa soko hilo la kisasa ambalo ujenzi wake umegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 2.843.
"Namwagiza Mkandarasi kuhakikisha kuwa hadi kufikia
Agosti 15 mwaka huu ujenzi wa soko hili uwe umekamilika na liwe
limekabidhiwa," Alisema Bw. Matinyi.
Bw. Matinyi ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
kuhakikisha hadi kufikia Agosti 31 mwaka huu maombi ya wafanyabiashara
walioomba vizimba na fremu za kufanyia biashara zao yawe yameshapitiwa tayari
kwa ajili ya kuwagawia.
Alisema soko hilo ni la kisasa ambalo litachukua
wafanyabiashara wengi tofauti na la awali ambalo lilikuwa limejengwa kwa mabati
hali ambayo ilikuwa ni hatarishi kwa wafanyabiashara. Kwamba kwa sasa soko hilo
litachukua zaidi ya wafanyabiashara 300 kwani lina vuizimba zaidi ya 136 na
fremu 150, na amempongeza na kumshukuru mkandarasi kwa kuongeza sehemu ya mama
lishe ambayo itakuwa na mama lishe 20.
"Kukamilika kwa Soko hili la kisasa pamoja na kuwa na
ubora, litakuwa na uwezo wa kuwahudunia wafanyabiashara wengi zaidi na hadi
sasa walioomba ni wafanyabiashara zaidi ya 3000," Alisema Bw. Matinyi.
Aidha, Bw. Matinyi pia ametumia ziara hiyo kuwahakikishia
wafanyabiashara wote ambao awali walikuwa wakifanya shughuli zao katika soko hilo
watarejeshwa wote na kisha ndio waaangalie maombi ya watu wengine, lakini pia
watakaokosa wataendelea kuwaboreshewa maeneo mengine, lengo ni kuhakikisha kila
mfanyabiashara anakuwa katika mazingira mazuri.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara watakaobahatika kufanya
biashara zao katika soko hilo kuhakikisha wanatunza miundombinu yake, mazingira
na kulipa kudi ya Serikali kwa uaminifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke, Bw. Elihuruma Mabelya amesema soko hilo la kisasa limejengwa kwa
gharama ya shilingi bilioni 2.843 na hadi sasa ujenzi wake umekamilika kwa
asilimia 99.
Amesema Halmashauri imejipanga kuhakikisha miundombinu ya
soko hilo inatunzwa ili kuwanufaisha wafanyabiashara kwa kupata kipato pamoja
na halmashauri kupata mapato pia.
Amewahakikishiwa wafanyabiashara kwamba ugawaji wa maeneo
utafanyika kwa haki na asitokee mtu yeyote wa kuwarubuni kwa kuwataka watoe
fedha ili wapatiwe maeneo.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashuri ya Manispaa ya Temeke
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kibonde Maji ambapo ndipo soko hilo lililopo
amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi
wa soko la kisasa.
0 Maoni