Mbunge wa Jimbo la Kibakwe ambaye pia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene ametoa ovyo kwa wananchi wanaoharibu vyanzo vya maji huku akiutaka
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kusimamia ipasavyo zoezi hilo.
Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi
kwa nyakati tofauti katika Vijiji cha Chang’ombe na Kidenge vilivyopo katika
Kata ya Luhundwa, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma kupitia mikutano ya hadhara ya
Mbunge huyo katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, ikiwa ni muendelezo wa kuelezea
utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo kufuatia mwananchi
mmoja kufanya shughuli za kilimo na ufugaji katika chanzo cha maji cha Igombo.
Amesema chanzo cha maji cha Igombo ni muhimu sana kwa
mustakabali wa maisha ya wananchi wa Luhundwa na Kibakwe kwa ujumla hivyo
kikiharibiwa kutakuwa na athari kubwa.
Mhe. Simbachawene ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa
kumuondoa mara moja mwananchi huyo ili kunusuru chanzo hicho cha maji ambacho
ni muhimu na tegemeo kwa wakazi wa maeneo hayo.
‘‘Maji ni uhai, siko tayari kuona vyanzo vya maji
vikiharibiwa kwa maslahi ya watu wachache, ni lazima tuchukue hatua ili iwe
funzo kwa wengine” amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Amesema athari za uharibifu wa mazingira zinagusa moja kwa moja masilahi ya wananchi wote bila kujali wewe ni nani katika jamii.
Ameongeza kuwa vyanzo vya maji visipolindwa Uongozi wao hautakuwa na maana kwani huko mbeleni watakuja kuulizwa na vizazi vijavyo.
Katika kulinda vyanzo hivyo vya maji, Mhe. Simbachawene
ameiagiza Halmashauri ya Mpwapwa kuunda kikosi maalum kitachokuwa na jukumu la
kulinda ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote
watakaobainika kuharibu vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mpwapwa, Mhe. George Fuime amemshukuru Mbunge huyo Mhe. Simbachawene kwa
kuzungumzia ulinzi wa vyanzo vya maji na kumhakikishia kuwa atasimamia ipasavyo
kwa kuhakikisha vyanzo hivyo vya maji vinalindwa.
Ameongeza kuwa yeye pamoja na timu yake ya Halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa watajitahidi kadri ya uwezo wao huku akitoa wito kwa wananchi
kutoa ushirikiano katika ulinzi wa vyanzo hivyo vya maji kwani bila maji hakuna
maisha.
Na Mwandishi wetu-Kibakwe
0 Maoni