Waziri Mkuu Majaliwa atoa neno Denmark kufunga ubalozi

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendela na jitihada za kuishawishi Denmark kuondoa azimio la kufunga ubalozi wake nchini.


Kufuatiza azima ya Denmark kufunga ubalozi wake nchini, serikali imetangaza kuwa, haina mgogoro na nchi hiyo na kwamba inaendelea na mazungumzo ili kuona Ubalozi wa nchi hiyo unaendelea na shughuli zake nchini.


Waziri Mkuu Majaliwa ametoa Kauli hiyo  Mei 11, 2023 bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Chakechake Ramadhani Suleiman Ramadhan (CCM) ambaye ametaka kujua kuhusu uvumi kuwa Serikali ya Denmark inaondoa ubalozi wake Tanzania kutokana na nchi hizo mbili kutokuwa na mahusiano mazuri. 


Waziri Mkuu amesema kuwa Denmark kwa sasa wanaweka Ubalozi kwenye nchi ambazo hazina usalama lakini Tanzania imekuwa na usalama hivyo wanatarajia kuondoa ubalozi wao 2024 lakini wanaendelea kuwashawishi waendelee kubaki.


Majaliwa  amekiri kuwa nchi hiyo imebadilisha sera zake katika Balozi zote kitu ambacho kimeifanya Tanzania kukosa sifa hizo na kusisitiza  hakuna mahusiano mabaya baina ya nchi hizi mbili na kwamba wamekuwa na mazungumzo mazuri kila wakati na mara ya mwisho ni wiki mbili zilizopita ambapo walizungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.


“Tanzania inayo mahusiano na nchi mbalimbali za kibalozi na tumeendelea kuwa na mahusiano mazuri sana na Denmark ikiwemo mahusiano ya kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi, wapo Watanzania wachache walioko Denmark wanaendelea na biashara zao kama kawaida bila ya hofu”.

Chapisha Maoni

0 Maoni