Sakata la baa kufungwa lachukua sura mpya NEMC, TPSF wavutana

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)  imelaani  kitendo cha wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC ) kufunga biashara 89 za baa na kumbi za starehe jambo ambalo limeathiri biashara nchini.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi  wa TPSF Raphael Maganga kwenye mjadala wa Mwananchi Twitter Space Mei  10,2023 alisema kuwa agizo la NEMC linarudisha nyuma jitihada za Serikali za Kukuza sekta binafsi na kusisitiza Serikali ya Tanzania inasimamia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na uwekezaji nchini BLUE PRINT ambayo inalenga kuboresha mazingira na kuondoa vikwazo kwenye biashara.



Maganga amebainisha kufungwa kwa biashara 89 kumeathari mnyororo mzima wa biashara ikiwemo, wasanii, viwanda vya vinywaji, chakula, wavuvi, wasafirishaji na wakulima hivyo kupoteza zaidi ya ajira 5,000 pamoja na upotevu mkubwa wa mapato kutokana na Biashara hizo kufungwa.


“TPSF inafahamu athari ya uchafuzi wa mazingira hasa wa kelele na madhara yake, na inaheshimu mifumo iliyopo inayolinda mazingira, ila utekeleaji wa sheria na kanuni unafaa kutekelezwa kwa weledi, haki na usawa kwa wote.” amesema Maganga



TPSF kama sauti ya Sekta Binafsi Nchini inashauri wafanyabiashara kuendelea kuweka mazingira bora na salama kwa watumiaji wa huduma zao huku wakifuata sheria zilizopo.


Sambamba na hilo, mamlaka husika waendelee kutoa elimu ya jinsi ya kutekeleza maelekezo na sio kufunga biashara kwani kufunga biashara kunachafua taswira nzima ya biashara nchini.


Pia ili kuhakikisha haki na usawa inapatikana mamlaka ya kufunga biashara nchini yabaki kwa mahakama au chombo maalamu chenye mamlaka ya kusikiliza pande zote.


NEMC yajibu 

Baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wadau kuhusu kufungiwa huko Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka amesema baada ya kutafakari athari za kiuchumi, wafanyabiashara 20 walioandika barua na kukiri makosa yao wamefunguliwa.


Mei 8, 2023, (NEMC) ilizifungia baa na kumbi za starehe 89 za majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma baada ya kubaini kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango vinavyotakiwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni