Taasisi tatu zaungana na serikali kulaani mauaji ya Dk. Sima Tarime

 

Chama cha Madktari Tanzania (MAT),Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), Kituo cha kutetea Haki za Binadamu (LHRC) wameungana kulaani mauaji ya Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Nyang'oto wilayani Tarime vijijini, Dk Isack Sima.


Katika matamko yao waliyotoa kwa nyakati tofauti kwa vyombo vya habari wametaka kufanyika kwa uchunguzi wa kifo chake na wote waliouhisika kuchukuliwa hatua kali.


Taarifa ya MAT

Katika taarifa ya MAT iliyotolewa Mei 7,2023 Rais wa MAT, Dk Deusdedit Ndilanha alisema "MAT imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha daktari na mwanataaluma mwenzetu kilichotokea katika wilaya ya Tarime vijijini mkoani Mara.

MAT imesema kwamba ulinzi na usalama wa raia yeyote katika nchi ni jukumu la vyombo vya dola ambavyo vinatakiwa kuhakikisha raia wake wanafanya kazi kwa waledi bila hofu wanaamini vyombo vya ulinzi na usalama vitawabaini na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria wale wote waliohusika na mauaji ya daktari huyo.



Wizara ya Afya 

Mei 6, 2023 Wizara ya Afya kupitia taarifa iliyotolewa kwa Umma na Kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa sekta hiyo, Aminiel Aligaesha ilieleza  kupokea  kwa masikitiko makubwa taarifa ya mauaji ya kikatili ya mtaalamu huyo wa afya.



“Wizara ya afya inalaani vikali kitendo hiki cha mauaji ya mwanataaluma ya udaktari na kitendo hiki hakikubaliki kwenye jamii,Serikali kupitia vyombo vyake inafanya ufuatiliaji dhidi ya mauaji hayo na taarifa rasmi itatolewa” ilieleza taarifa hiyo


Taarifa ya MCT

Mei 6,2023 Baraza la Madaktari Tanganyika lilitoa tamko lililosainiwa na msajili wa baraza hilo Dk David Mzava ambapo limewasihi wanataaluma wote kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki ambacho vyombo vya dola vinafanya uchunguzi wa mauwaji hayo ya kinyama.



LHRC

Mei 7,2023 Katika taarifa ya Kituo cha kutetea Haki za Binadamu iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Felista Mauya imesema Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani na kukemea matukio ya mauaji yanayoendelea nchini kwani matukio hayo yanapoka haki ya kuishi. 


Ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2022 imeonyesha uwepo wa matukio kadhaa ya mauaji yanayofanywa na watu mbalimbali ikiwemo watu wasiojulikana pamoja na matukio ya kujichukulia sheria mkononi. Matukio hayo yameripotiwa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Mkoa wa Mara.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kikatili bali kuendelea kulinda na kuheshimu haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi.


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa rai kwa Jeshi letu la Polisi kufanya uchunguzi wa jambo hili na kuhakikisha waliofanya uhalifu huo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.


Mei 3, 2023. Dk Sima alikutwa ameuwawa  kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana wakati akitoka kituo chake cha kazi Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini mkoani Mara.

Chapisha Maoni

0 Maoni