Nchi za SADC zaweka msimamo kusitishwa mzozo DRC

 

Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umetoa wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.


Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo wa dharura uliofanyika Mei 8, 2023 jijini Windhoek nchini Namibia ambapo umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya uchaguzi.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus imesema kufanyika kwa mkutano huo kunatokana na mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na watu wenye silaha kali nchini DRC ambao kwa vipindi tofauti wamekuwa wakisababisha maafa.


Mkutano  huo unatarajiwa kufanyika tena Desemba 2023 umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi wa Congo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla.



Taarifa hiyo imeeleza mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la SADC kutoka kikosi cha kudumu cha jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama.


Washiriki walikuwa ni Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervention Brigade (FIB).



Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Namibia Dk Hage Geingo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa DRC Félix Tshisekedi, Waziri wa Mahusiano ya Mambo ya Nje wa Angola, Balozi Tete Antonio, Waziri wa Ulinzi wa Malawi, Harry Mkandawir pamoja na Balozi wa Zambia chini Namibia Stephen Katuka.

Chapisha Maoni

2 Maoni

Bila jina alisema…
Piga hao m23 Rwanda wanamkono hapo
Bila jina alisema…
Hongera mama samia unasimamia show kila kona