Makampuni 300 yaomba mradi wa barabara ya kulipia Kibaha-Chalinze

 


Zaidi ya makampuni 300 ya nje ya nchi, yameomba kufanya mradi wa ujenzi wa barabara kuu (Highway) kipande cha Kibaha- Chalinze, utakaogharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 350 sawa na shilingi bilioni 800 za Tanzania.

Ujenzi wa kipande hicho pia utaongezwa kutoka Chalinze hadi Morogoro kupitia Ubia wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP), katika kujaribu kuiondolea mzigo Serikali wa mahitaji ya miundombinu unaotokana na ongezeko la watu na idadi ya watu wanaohamia mijini.

Akiongea na wahariri katika mkutano wake kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Kamishna wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi Kamishna David Kafulila amesema lengo la PPP ni kupunguza utegemezi wa Serikali katika miradi mikubwa.

“Kwa upande wa kipande cha Kibaha- Chalinze tupo kwenye tathimini na tayari makampuni ya nje zaidi ya 300 yamejitokeza kuomba kufanya mradi huo, hivyo baada ya muda si mrefu ujenzi wake wa barabara nne (four lanes) utaanza.

Amesema kukamilika kwa ujenzi huo wa barabara kuu ya kulipia kipande cha Kibaha- Chalinze na kile cha Chalinze-Morogoro kutapunguza foleni kwa kuwa baadhi ya magari yatapungua katika barabara ya umma, na kuokoa muda na fedha.

“Watanzania wanapaswa kuanza kuzoea barabara za kulipia, kwani hazinatofauti na kuamua kutumia shule ya binafsi ama ya umma, ama hospitali binafsi na hospitali za umma na zote hizo zinagharama zake kwa mtumiaji,” amesema Kamishna Kafulila.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Igawa-Tunduma Kamishana Kafulila amesema tayari ipo kampuni moja imejitokeza kutaka kujenga mradi huo, hivyo hakuna haja tena ya Serikali kuanza kutafuta mwekezaji mwingine.

Akizungumzia suala ya sharia ya PPP kufanyiwa marekebisho mara kwa mara Kamishna Kafulila amesema hali hiyo inatokana na ushindani uliopo na nchi nyingine, hivyo ni vyema kufanya marekebisho ili kuvutia zaidi wawekezaji.

Pamoja na mambo mengine Kamishna Kafulila amesema kwa mara ya kwanza katika historia Serikali imeilipa kampuni ya Kimataifa ya Moody’s kufanya tathimini ya afya yetu ya uchumi na uwezo wetu wa kukopa, jambo ambalo litasaidia sana nchi kuaminika na kupata mikopo kirahisi.  

Chapisha Maoni

0 Maoni