Watumishi wa Wizara ya Fedha Watakiwa Kuendelea Kutoa Huduma kwa Weledi

 

Na. Asia Singano na Saidina Msangi, WF – Dar Es Salaam

Watumishi wa Wizara ya Fedha na Taasisi zake, wametakiwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kwa weledi ikiwemo kutoa elimu kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji pamoja na kuendelea kueleza wananchi wanaotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Wizara ya Fedha.

Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, alipotembelea, Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Aliwapongeza watumishi hao kwa namna walivyojipanga kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wanaotembelea katika Banda hilo kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma mbalimbali na kuelezwa kuhusu huduma zinazotolewa na majukumu yanayotekelezwa na Wizara ya Fedha.

''Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, hakikisheni wananchi wanaowatembelea wanapata huduma nzuri endeeleni na kazi, asante'' alisema Bw. Joshua.

Aidha aliwakaribisha wananchi kutembelea Banda la Wizara ya Fedha ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupata elimu kuhusu masuala ya kifedha, huduma za wastaafu wanaolipwa na Hazina, fursa za uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji ikiwemo UTT Amis na kufahamu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na wizara hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, Mkazi wa Dar es Salaam, Bw. Bajunwa Libent, alisema amepata uelewa mkubwa kuhusu majukumu ya Idara mbalimbali pamoja na taasisi za Wizara ya Fedha, hasa katika nafasi yake katika kuandaa na kusimamia sera za maendeleo na usimamizi wa fedha nchini, ambapo elimu hiyo imemwezesha kufahamu fursa mbalimbali zinazotokana na sera hizo, hususan kwa vijana wanaotaka kushiriki katika shughuli za uwekezaji, biashara na maendeleo ya uchumi.

Bw. Libent alisema pia amefurahi kusikia taratibu za kushiriki katika zabuni za Serikali, ikiwemo namna ya kuomba zabuni na vigezo vinavyotakiwa ili kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotolewa na Serikali.

"Nawahimiza wananchi wenzangu kutembelea banda la Wizara ya Fedha, katika kipindi chote cha maonesho ili kujipatia taarifa sahihi kuhusu huduma, sera na fursa mbalimbali zinazotolewa, kwa kuwa elimu hii ni muhimu katika kutuwezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi" alisema Bw. Libent.

Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam ni maonesho ya 50 tangia kuanza kwa Maonesho hayo.



Chapisha Maoni

0 Maoni