Mameneja wa TARURA wa Mikoa nchini wametakiwa kuwa na jukwaa moja na mpango kazi na Wakufunzi wasaidizi ili waongee lugha moja katika kufanikisha Mpango wa Matengenezo ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM).
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mtendaji
Mkuu wa TARURA, Mhandisi Edward Amboka wakati akifunga mafunzo ya
kuwajengea uwezo Mameneja wa Mikoa yaliyofanyika jijini
Mwanza.
Mhandisi Amboka amesema kwamba mpango kazi wa
pamoja utaweza kufanikisha kutekeleza mpango huo ambao unaenda
kumuongezea kipato cha ziada mwananchi wa kawaida na kumsaidia
kuinuka kiuchumi.
“Kuna kazi za kwenda kufanya
mtakaporudi kwenye maeneo yenu ya kazi na ili "mscore"
vizuri lazima mkakae na wakufunzi wasaidizi na mtumie weledi wenu ili
mfaulu utekelezaji wa mpango huu”.
Amesema kupitia
CBRM serikali kupitia TARURA inatarajia kunusuru barabara nyingi
hususan za vijijini ambazo zinawasaidia wananchi kufika mashambani
msimu wa kilimo na pia kusafirisha mazao yao hata kama bado kuna
mvua.
“Tanzania tuna mtandao mkubwa wa barabara,
serikali inatafuta vyanzo mbalimbali vya kukwamua barabara zake na
kuwafikia wananchi wake kwani barabara zinapoharibika wananchi
hushindwa kupita na kupata huduma mbalimbali za kijamii”.
Hata
hivyo, amesema mpango huo licha ya kuwaongezea kipato cha ziada
mwananchi unaenda kuongeza umiliki wa miundombinu kwa wananchi ili
kuondokana na dhana ya ulinzi wa miundombinu ni wa serikali bali
wanaposhirikishwa katika matengenezo ya kawaida wataona barabara hizo
ni mali yao na watazilinda na kuzitunza.
Awali
akimkaribisha Kaimu Mtendaji Mkuu, Meneja wa Barabara TARURA,
Mhandisi Oscar Mlekwa amewapongeza waratibu wa mpango huo kwa hatua
kubwa waliofikia ambayo imeanza kuonesha mafanikio na kusema kuwa
serikali inatupia macho kazi hizo ambazo zinajumuisha na kuwagusa
wananchi na kuwainua kiuchumi.
Naye, Mratibu wa CBRM,
Mhandisi Richard Missa amewaomba washiriki wa mafunzo hayo kutoa
taarifa kwa makini na kwa wakati ili kuwezesha kufikia malengo ya
mpango huo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu kutoka
Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Dampu Ndezako amesema mpango wa
CBRM ni jitihada za serikali za kuondoa hali ya umaskini kwa wananchi
wake wa chini kwa kutumia vikundi ambapo wananchi wanaenda kupata
fursa ya kuzalisha kipato na kuweza kujitegemea.

.jpeg)
0 Maoni