Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaohusika na vitendo hivyo.
Katika taarifa yake kwa umma, JWTZ imesema kuwa ina jukumu la kulinda usalama wa nchi na wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taifa Sura ya 192.
Jeshi hilo limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na matukio yoyote ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani.
Aidha, wananchi wamehimizwa kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vya uchochezi ili kudumisha utulivu nchini.
JWTZ pia limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka, Katiba na mamlaka ya nchi sambamba na kushirikiana na wananchi katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Sylvester Mangure.

0 Maoni