Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wamepongeza serikali kwa jitihada zake katika kuzingatia na kulinda haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Pongezi hizo zimekuja kufuatia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya kulinda haki hizo kwa mujibu wa mikataba ya kikanda na kimataifa inayotekelezwa nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU) na mgombea urais mwaka 2025, Majalio Kyara, amebainisha kuwa mwelekeo wa sasa wa ulinzi wa haki za binadamu nchini ni mzuri. Kyara alisisitiza kuwa mapungufu yanayojitokeza ni sehemu ya ubinadamu, hivyo akashauri wananchi kutii sheria bila shuruti ili kulinda haki, huku akiongeza kuwa pale panapokuwa na changamoto, marekebisho yanapaswa kufanyika kwa utaratibu na mipango thabiti kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD), Hassan Doyo, amekubaliana na kauli ya Rais Samia akieleza kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2021, Rais amekuwa akitekeleza falsafa ya 4R na kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya sheria, ikiwemo uundaji wa Tume ya Haki Jinai na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Hata hivyo, Doyo alishauri serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya vyombo vinavyosimamia haki ili kupunguza ucheleweshwaji wa kesi, huku akisisitiza kuwa haki za binadamu ni suala mtambuka linalohitaji uelewa wa wananchi pia.
Naye Katibu Mkuu wa Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, amesema kuwa mifumo ya haki nchini ipo vizuri na inasimamiwa vyema na Rais Samia, jambo ambalo limechangia kuwepo kwa umoja na utulivu. Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK) mwaka 2025, David Mwaijojele, amemhimiza Rais kuendelea kutekeleza kauli hiyo kwa vitendo ili kutatua kabisa malalamiko ya kuminywa kwa haki za binadamu, akisisitiza kuwa utawala wa haki ni nguzo muhimu katika kupunguza umaskini.
Wachambuzi wa siasa, Richard Mbunda na
Nathan Kimaro, wameunga mkono hatua za serikali huku wakishauri kuendelea
kufanyiwa kazi kwa tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu. Kimaro
aliongeza kuwa anaamini Rais Samia ana mamlaka na uwezo wa kuweka nchi sawa kwa
kuelekeza watendaji wake kusimamia mifumo kwa haki, hatua ambayo anaamini
itasaidia kumaliza malalamiko na tuhuma zote za ukiukwaji wa haki za binadamu
zinazoweza kujitokeza ndani na nje ya nchi. Habari hii imeandikwa na Ramla
Hamidu na Eva Sindika.

0 Maoni