Na. Faustine Gimu,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma
Matumizi ya Sayansi ya Mabadiliko ya Tabia imeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu
katika kuimarisha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango, kwa kuwa husaidia
kubaini sababu zinazochangia maamuzi ya watu kuhusu afya na kuwezesha kubuni
afua zinazojibu mahitaji halisi ya jamii.
Akizungumza wakati wa Mafunzo ya Sayansi ya Mabadiliko ya Tabia kwa Waratibu wa
Elimu na Hamasa ya Afya kwa Umma, Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Halmashauri,
Mkoa na Vituo vya kutolea Huduma za Afya mkoani Kigoma, Mganga Mkuu wa Mkoa ,
Dkt. Damas Kayera, amesema mafanikio katika kuongeza matumizi ya huduma za
uzazi wa mpango yanategemea matumizi ya ushahidi wa kisayansi unaoeleza kwa
nini watu hufanya au hushindwa kufanya maamuzi yanayohusu afya zao.
"Sayansi ya Mabadiliko ya Tabia inatuwezesha kuelewa sababu za tabia za
watu na kubuni afua zinazozingatia ushahidi. Hii ndiyo njia sahihi ya kuongeza
matumizi ya huduma za uzazi wa mpango na kuboresha afya ya uzazi, mama na
mtoto," amesema Dkt. Kayera.
Amewataka Waratibu wa elimu na hamasa ya afya kutumia maarifa waliyopata katika
mafunzo hayo kubuni na kutekeleza afua zinazozingatia mazingira halisi ya
jamii, ili kuongeza uelewa, kuondoa dhana potofu na kuimarisha matumizi ya
huduma za uzazi wa mpango.
Mratibu wa Mafunzo hayo, Bw. Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya amesema
mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika kuhakikisha huduma za uzazi wa Mpango
zinakuwa bora zaidi kwa kuongeza hamasa.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani(WHO) Tanzania
Kitengo cha Elimu ya Afya wakati wa Magonjwa ya Mlipuko na Dharura Bw.Jerry
Bikyeombe amesema Mafunzo hayo ni muhimu katika kuhakikisha jamii inakuwa na
elimu sahihi na kufanya maamuzi sahihi ya kupata huduma za afya hususan Uzazi
wa Mpango.
Kwa upande wao baadhi ya Wanufaika wa Mafunzo hayo akiwemo Mratibu wa Huduma za
Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Kigoma Bernadeta Peter pamoja na
Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Erick Ernest
wamesema mafunzo hayo yatakuwa na chachu kubwa katika elimu ya Afya ya Uzazi wa
Mpango Mkoa wa Kigoma.


0 Maoni