Serikali yaanza ujenzi wa maabara ya kisasa ya upimaji sampuli za madini

  

Kufuatia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), hatua hiyo inakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara ya madini kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Julai, 2026 na Waziri wa Madini, Mh.Anthony Mavunde (Mb) alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maabara ya GST uliopo Kizota, Jijini Dodoma. 

"Tunamshukuru Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huu wa kisasa, unaokwenda kuifanya Nchi yetu kuwa kinara na mahiri katika utoaji wa huduma za maabara za madini" 

"Mradi huu pia unakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara kwa Nchi za Afrika ya Mashariki na Kati, kutokana na ubora wa huduma hizo kuwa za kimataifa" alieleza Waziri Mavunde. 

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa kwa muda mrefu wachimbaji wadogo wamekuwa wakipata changamoto ya upimaji wa sampuli zao kwenye maabara, hali iliyopelekea kushindwa kufanya shughuli zao kiufanisi. 

Mavunde alisisitiza kuwa ujio wa maabara hiyo ya kisasa unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za wachimbaji ikiwa ni pamoja na kuhudumia wachimbaji wengi zaidi kwa ubora wa kimataifa. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania, Mhandisi Ally Samaje alieleza kuwa ujenzi wa mradi huo wa maabara unagharimu shilingi bilioni 14.3 na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo unataraji kukamilika ifikapo Mwezi Septemba, 2027. 

Aidha, aliongeza kuwa maabara hiyo ikikamilika itakuwa ni ya kisasa na inakwenda kuhudumia wateja wengi wa ndani na nje ya Nchi.



Chapisha Maoni

0 Maoni