Rais wa Singapore kuanza ziara ya kitaifa nchini kesho

 

Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, anatarajiwa kuwasili nchini leo jioni kwa ziara ya kitaifa, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kesho, tarehe 09 Juni, 2026, Rais Shanmugaratnam atapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam, na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hao wawili watafanya mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore katika maeneo mbalimbali hususan biashara, uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi, pamoja na uchumi wa kidijitali.

Mazungumzo hayo yatafuatiwa na utiaji saini wa mikataba na Hati za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, na mkutano wa pamoja na waandishi wa habari. Baadaye siku hiyo, Rais Shanmugaratnam, akiambatana na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia, atashiriki Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Singapore litakalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Jukwaa hilo litawakutanisha viongozi wa sekta ya umma na binafsi kutoka nchi zote mbili kwa lengo la kujadili fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi. Aidha, Rais Shanmugaratnam atahutubia mhadhara wa wazi (Open Lecture) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wenye mada ihusuyo “Uwekezaji katika Vichocheo vya Ukuaji Jumuishi,” ambapo ataeleza uzoefu wa Singapore katika kujenga uchumi shindani unaojumuisha wananchi wote.

Tarehe 10 Juni, 2026, Rais Shanmugaratnam atafanya ziara Zanzibar na kukutana kwa mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kabla ya kurejea Dar es Salaam na kuondoka nchini baada ya kukamilisha ziara yake.

Ziara hii ya kitaifa inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Singapore, pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji, maendeleo ya ujuzi na ubadilishanaji wa uzoefu katika maeneo ya kimkakati kwa maendeleo ya nchi zote mbili. Ziara ya Rais Shanmugaratnam inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore.

Taarifa Na. Bakari S. Machumu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Chapisha Maoni

0 Maoni