Na. Mwandishi Wetu (TBN) Dar es Salaam
Mikataba na hati za makubaliano manane (8) zilizosainiwa kati ya Tanzania na Urusi, ndizo zilizoweka msingi mkuu wa ushirikiano mpya wa kiuchumi, kijamii na kiteknolojia unaotarajiwa kupandisha hadhi ya nchi hizi mbili.
Makubaliano haya makubwa, ambayo ni matunda ya moja kwa moja ya ziara ya kihistoria ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, yanajenga daraja imara la maendeleo katika sekta tisa za kipaumbele: kilimo, elimu, nishati, madini, viwanda, utalii, usafirishaji, uchumi wa kidijiti, pamoja na biashara na uwekezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameanika hadharani undani wa makubaliano hayo manane yanayobeba mustakabali wa nchi:
Kutoka Diplomasia ya Lugha Hadi Mapinduzi
ya Afya na Elimu ya Juu
Katika makubaliano ya kwanza, Tanzania na
Urusi zimeamua kutumia lugha kama silaha ya kidiplomasia. Kupitia
hati ya ushirikiano kati ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na
Chuo Kikuu cha Mahusiano ya Kimataifa cha Urusi (MGIMO), lugha ya
Kiswahili itazidishwa kasi ya kufundishwa nchini Urusi, huku Tanzania
nayo ikijipanga kuanza kufundisha Kirusi kupitia Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM).
Makubaliano ya pili yamejikita kwenye sekta ya
afya, ambapo Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) kimeingia ubia na
taasisi mbili za afya za Urusi kwa ajili ya kubadilishana utaalamu wa
matibabu na kuongeza nguvu katika uzalishaji wa dawa nchini.
Kwenye
upande wa elimu, makubaliano ya tatu na ya nne yanakuja kutatua
changamoto za ajira na teknolojia ya kisasa:
Wizara za Elimu
za nchi zote mbili zimesaini makubaliano ya kutambua vyeti na tuzo za
kitaaluma zinazotolewa Urusi, hatua itakayowawezesha Watanzania
waliosoma nchini humo kupata ajira kwa urahisi nyumbani.
Taasisi
ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imesaini mkataba na Chuo cha
Urafiki cha Urusi kuanzisha programu za pamoja za Shahada ya Kwanza
na Uzamili katika fani za kisasa kabisa duniani—ikiwemo Sayansi ya
Takwimu, Mfumo wa Anga, Akili Unde (AI), na Ujifunzaji wa Mashine
(Machine Learning).
Kuvutia Mitaji ya Magharibi, Siri za
Nishati na Ajira za Vijana
Makubaliano ya tano na ya sita
yanalenga kufungua milango ya mitaji mikubwa. Kupitia Mamlaka ya
Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), nchi
imepewa fursa ya kuhamasisha uwekezaji hadi kuelekea mataifa ya
Ulaya.
Zaidi ya hapo, Tanzania imeingia ushirikiano na
Kampuni ya Roscongress ya Urusi—miamba ya kuandaa makongamano ya
kimataifa—kwa lengo la kutengeneza miradi ya ubia na kuvutia
wawekezaji sio tu kutoka Urusi, bali pia kutoka nchi za
Magharibi.
Mkataba wa saba uligusa sekta nyeti ya nishati,
ambapo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Mantra
Tanzania Ltd (Kmapuni tanzu ya Shirika la Nyuklia la Urusi, Rosatom)
zimesaini makubaliano ya kulinda na kutunza siri za taarifa za
kimkakati katika miradi ya nishati.
Kama kilele cha
makubaliano hayo, kubaliano la nane ni mpango kabambe wa miaka mitano
unaolenga kukuza uchumi na kuzalisha fursa za ajira kwa vijana wa
Kitanzania nchini Urusi.
"Haya ni matunda halisi ya
kiuchumi yaliyotokana na maono ya mheshimiwa Rais," alisisitiza
Profesa Kitila Mkumbo, akibainisha kuwa utekelezaji wa makubaliano
haya unaenda kuweka alama ya kudumu katika soko la ajira na uwekezaji
nchini.

0 Maoni