Tume
ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa
imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kutoa
elimu na kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kupitia Maonesho ya
Utafiti, Ubunifu na Huduma kwa Jamii yanayoendelea katika viwanja vya
Garden Posta, Manispaa ya Iringa.
Maonesho hayo,
yaliyowakutanisha taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi,
yanalenga kuelimisha wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi
hizo pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo
mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya madini.
Akizungumza
katika maonesho hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mjiolojia
Bertha Luzabiko, amesema ushiriki wa Tume ya Madini unalenga kutoa
elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za madini, taratibu za upatikanaji
wa leseni za madini na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta
hiyo.
Amesema Mkoa wa Iringa una rasilimali mbalimbali za
madini zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi, hivyo
wananchi na wawekezaji wanapaswa kuzitumia fursa hizo kwa kufuata
sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta ya madini
nchini.
Awali akifungua maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Mhe. Kheri James, aliwataka wananchi kutumia maonesho hayo kujifunza,
kufanya ubunifu na kunufaika na fursa zinazotolewa na taasisi
mbalimbali kwa maendeleo yao na ya taifa.
Maonesho hayo
yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na
Chuo Kikuu cha Mkwawa, yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya
taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi katika kuchochea maendeleo
kupitia utafiti, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa jamii.


0 Maoni