Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Itikadi,
Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema sehemu kubwa ya
machafuko na migogoro inayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika
huchochewa na watu wachache wanaotumiwa kwa maslahi binafsi ili
kuvuruga amani na utulivu wa mataifa yao.
Kihongosi alitoa
kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
eneo la Kilombero, jijini Arusha, Mei 7, alipokuwa akihitimisha ziara
yake mkoani humo.
Alisema historia inaonyesha kuwa hata wakati
wa ukoloni kulikuwepo watu waliotanguliza maslahi yao binafsi na
kushiriki katika vitendo vilivyowadhuru Waafrika wenzao kwa manufaa
ya fedha na madaraka.
“Kuna watu wanalipwa fedha nyingi kwa
ajili ya kuchochea migogoro ndani ya bara la Afrika. Ndiyo maana hata
wakati wa ukoloni walikuwapo wasaliti waliowauza Waafrika wenzao kwa
kupewa vipande vya fedha na madaraka,” alisema
Kihongosi.
Aliwataka wananchi kuwa makini na watu wanaotumia
mbinu mbalimbali kupotosha ukweli na kueneza chuki katika jamii kwa
malengo ya kuvuruga mshikamano wa kitaifa.
Kihongosi alisema
ni muhimu kwa wananchi kuendelea kudumisha umoja, upendo na
mshikamano ili kulinda amani ambayo ni msingi wa maendeleo ya
nchi.
Aidha, alionya dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya
kisiasa, akisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiyatumia kueneza
chuki na kuhamasisha machafuko, jambo ambalo linaweza kuhatarisha
maendeleo na ustawi wa jamii.
Alisisitiza kuwa siasa zinapaswa
kutumika kama chombo cha kujenga maridhiano, kuhimiza maendeleo na
kuimarisha mshikamano wa wananchi badala ya kuzalisha migawanyiko
ndani ya jamii.

0 Maoni