Mkuu wa Wilaya ya Ulanga,
Khamana Juma Simba, amewahimiza vijana wa wilaya hiyo kulinda amani
ya taifa ili kila mwananchi awe huru kufanya shughuli zake za
maendeleo, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo
kwa amani.
Simba alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa
Jukwaa la Vijana (Youth Platform), linalolenga kuwakutanisha vijana
kutoka makundi mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya maendeleo
na fursa zinazowahusu.
“Mimi niwaombe vijana wa Wilaya ya
Ulanga kutoka maeneo yote twende tukawa walinzi wa wilaya yetu,
nendeni mkawa walinzi wa nchi yetu na walinzi wa sisi wenyewe,
tutapunguza mambo yote mabaya,” alisema Simba.
Aidha,
aliwataka vijana kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na Halmashauri
kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na kujenga maisha bora, huku
akiwahimiza kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika jamii.
Pia,
aliwaasa vijana kutotumia vibaya mitandao ya kijamii, badala yake
waitumie kama chombo cha kujifunza, kufanya biashara na kujiongezea
kipato.
“Mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo muhimu ya
maendeleo ikiwa itatumika kwa malengo chanya. Wapo watu wanaofanya
biashara kupitia mitandao hiyo na kupata riziki zao,” alisema.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Salim Hashim, aliwataka
vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia
Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ili kujikwamua kiuchumi.
Hashim
alisema ofisi yake imeandaa mpango maalumu wa kuwawezesha vijana
kupitia mikopo isiyo na riba, hatua inayolenga kuwasaidia kukuza na
kuendeleza biashara zao pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji
mali.
Alisisitiza kuwa uwezeshaji wa vijana kiuchumi ni moja
ya njia muhimu za kupunguza changamoto za ajira na kuongeza ushiriki
wao katika maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla.

0 Maoni