Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaapisha majaji wa Mahakama Kuu aliowateua hivi karibuni kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya
kuwaapisha majaji hao, Rais Dkt. Samia amewataka kutekeleza majukumu
yao kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo, huku wakitambua uzito wa
dhamana waliyopewa ya kusimamia haki za wananchi na maslahi ya Taifa
kwa ujumla.
Amesema uteuzi wa majaji katika ngazi hiyo ya juu
ya Mahakama ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mfumo wa
utoaji haki nchini, ikiwemo kukabiliana na ongezeko la mashauri
pamoja na mahitaji ya wananchi ya kupata haki kwa wakati.
Katika hatua nyingine,
Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuiwezesha Mahakama ili
kuongeza ufanisi katika utoaji haki na kuhakikisha wananchi wanapata
huduma za kimahakama kwa wakati na kwa usawa.
Aidha, amewataka majaji hao
kuzingatia maadili ya kazi, nidhamu na busara katika maamuzi yao ili
kuendelea kulinda hadhi ya Mahakama pamoja na kuimarisha imani ya
wananchi kwa mhimili huo wa utoaji haki.
Majaji walioapishwa ni Imani Daud Aboud, Rabia Hussein Mohamed, Yose Joseph Mlyambina, Immaculata Kajetan Banzi, Cyprian Phocas Mkeha, Yohane Bokobora Masara, Juliana Laurent Masabo, Abdi Shaaban Kagomba na Mzee Ibrahim Ibrahim.



0 Maoni