Mkoa wa Mtwara
umeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji katika
sekta ya chumvi kutokana na uwepo wa fukwe zinazofaa kwa uzalishaji,
maboresho ya mazingira ya biashara na ongezeko la uzalishaji
linalofikia takribani tani 90 kwa majaruba manne katika baadhi ya
maeneo ya uzalishaji.
Kutokana na hatua hiyo, wachimbaji na
wazalishaji wa chumvi wameanza kunufaika na fursa mpya za kiuchumi
kupitia kuongezeka kwa uzalishaji, ajira na upanuzi wa maeneo ya
uzalishaji.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Winnifrida Mrema, amesema sekta ya chumvi
mkoani humo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuimarika kwa
shughuli za uzalishaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa
katika uchakataji wa chumvi.
Amesema maboresho hayo yanalenga
kuongeza ubora wa chumvi kwa matumizi ya majumbani, viwandani na
mifugo, huku yakichochea ajira kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka
mashamba ya chumvi.
“Mtwara ina mazingira rafiki kwa
uzalishaji wa chumvi na Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji
katika sekta hii ili kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa
ujumla,” amesema Mrema.
Katika Kijiji cha Mnete, Kata ya
Nalingu Halmashauri ya Mtwara Vijijini, msimamizi wa mashamba ya
chumvi, Salum Amani, amesema mashamba hayo yanamilikiwa na Zamda
Khatibu na yana leseni mbili za uvunaji chumvi pamoja na majaruba 24
yanayotumika kwa uzalishaji.
Amesema kwa sasa wanaendelea na
shughuli za usafishaji wa majaruba baada ya msimu wa mvua ili
kuruhusu maji ya chumvi kuingia tayari kwa uzalishaji mpya.
Kwa
mujibu wa Salum, uzalishaji wa chumvi hutegemea hali ya hewa, ambapo
jua kali huwezesha chumvi kukauka ndani ya siku 30, huku hali ya
baridi ikifanya mchakato huo kuchukua hadi siku 40.
“Kwa
kawaida majaruba manne huzalisha takribani tani 90 za chumvi kwa
msimu mmoja, huku shughuli hizi zikitoa ajira kwa wafanyakazi tisa
katika eneo hili,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Chama cha Wazalishaji Chumvi Mkoa wa Mtwara na Mwenyekiti wa Kamati
ya Chumvi kupitia FEMATA, Khalfan Nassoro, amesema kupunguzwa kwa
gharama ya ada ya pango ya leseni za chumvi kutoka Shilingi 45,000
hadi Shilingi 20,000 kumeongeza uwezo wa wazalishaji kupanua maeneo
ya uzalishaji.
Amesema hatua hiyo imeongeza matumaini kwa
wawekezaji na wachimbaji wadogo, huku akisisitiza kuwa mazingira bora
ya uwekezaji yataifanya Mtwara kuwa kitovu kikuu cha uzalishaji wa
chumvi nchini.
Nassoro amesema pia ukuaji wa sekta hiyo
unaweza kuchochea ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya chumvi na
hivyo kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.



0 Maoni