JESHI la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari baada ya kufanikiwa kudhibiti mipango ya baadhi ya watu waliokuwa wakihamasisha vitendo vya kihalifu kupitia maandamano yasiyofuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Akizungumza katika taarifa kwa umma, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema kwa nyakati tofauti jeshi hilo limekuwa likitoa taarifa za kiusalama kuhusu makundi yaliyokuwa yakipanga na kuhamasisha vitendo vya uhalifu, ikiwemo kupanga kuua watu, kuchoma moto shule ili kuzua hofu kwa wazazi na walezi, kulipua transfoma za TANESCO, kufunga barabara na kuwanyang'anya askari silaha.
Amesema mipango hiyo ilikuwa ikifanyika kupitia vikao vya ana kwa ana, kurubuni vijana, pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe na kufanya mikutano kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Misime amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama lilifanikiwa kuwafuatilia wahusika hao na kuwakamata baadhi yao, huku idadi yao ikitangazwa Julai 9, 2026. Aliongeza kuwa baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 26, 2026, huku wengine wakiendelea kutafutwa.
Amewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kuzingatia maelekezo ya vyombo vya dola na kutoshiriki katika vitendo hivyo, akisema hatua hiyo imechangia kuendelea kuwepo kwa hali ya utulivu na usalama nchini.
Misime amesema katika kipindi ambacho kulikuwa na viashiria vya vitendo hivyo vya kihalifu, Jeshi la Polisi lilikuwa likipokea taarifa kutoka vyama mbalimbali vya siasa na baadhi ya wabunge kuhusu nia ya kufanya mikutano ya hadhara na vikao katika majimbo yao.
Amesema kutokana na jukumu la Jeshi la Polisi la kusimamia usalama wa mikutano hiyo, wahusika waliitwa na kushauriwa kuahirisha shughuli hizo kutokana na hali ya kiusalama iliyokuwapo wakati huo.
Hata hivyo, amesema kutokana na hali ya usalama kuendelea kuwa shwari, Jeshi la Polisi litaendelea kupokea taarifa za nia ya kufanya mikutano ya hadhara, na kuwahimiza wote wenye nia hiyo kuwasilisha taarifa kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Misime ametoa wito kwa wananchi kuendelea kukataa vitendo vya uhalifu na kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya kupanga au kuhamasisha uhalifu ili hatua za haraka zichukuliwe kabla ya matukio hayo kukua, akisisitiza kuwa amani na usalama ni msingi muhimu wa maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.

0 Maoni