Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum amesema jumuiya hiyo inapinga kauli zilizotolewa na baadhi ya maseneta wa Bunge la Marekani waliodai kuwa Tanzania si salama na kwamba kuna vitendo vya ubaguzi wa kidini pamoja na baadhi ya waumini kutotendewa haki.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Sheikh Alhad amesema madai hayo ni uzushi usiokuwa na msingi na kwamba kauli hizo zina lengo la kuchochea migawanyiko na kuvuruga amani iliyopo nchini. Amesisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuwa mfano wa mshikamano wa kidini kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Katibu wa JMAT, Askofu Israel Maasa amesema kwa zaidi ya nusu karne Watanzania wa dini zote wamekuwa wakiishi kwa amani, utulivu na kuheshimiana bila kujali tofauti zao za kiimani.

Askofu Maasa amesema JMAT, ambayo inawakutanisha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini za Kiislamu, Kikristo na nyinginezo, itaendelea kuhamasisha maridhiano, mshikamano na umoja wa kitaifa ili kulinda amani ya nchi.

Aidha, jumuiya hiyo imeeleza kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha haki, uwajibikaji na maridhiano nchini, ikiwemo hatua ya kuunda Tume ya Uchunguzi pamoja na Tume ya Kijinai kuhusu matukio ya kabla na baada ya Oktoba 29, 2025, kwa lengo la kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa haki na Katiba Mpya kama alivyoahidi.

#SisiNiWamoja