Wakati Taifa likiingia katika mwaka 2026, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa dira mpya
inayochanganya mageuzi makubwa ya kiuchumi na diplomasia ya kisasa, akilenga
kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji na ustawi barani Afrika.
Utekelezaji wa Ahadi na Ilani
Rais Samia amebainisha kuwa serikali yake imejipanga kutoa
mrejesho wa kina wa utekelezaji wa ahadi za siku 100 za kampeni ifikapo mwezi
Februari 2026. Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa kwa vitendo, huku kipaumbele kikiwa ni
kuboresha maisha ya jamii na kufungua fursa sawa za kiuchumi na kisiasa kwa
kila mwananchi.
Uchumi Imara na Dira ya 2050
Katika kile kinachoashiria uthabiti wa uongozi wake, Rais
Samia ameanika mafanikio makubwa ambapo Pato la Taifa (GDP) limekua hadi
asilimia 5.8 mwaka 2025, likitoka asilimia 5.2 ya mwaka uliotangulia. Ukuaji
huu unachagizwa na uwekezaji wa kimkakati katika sekta za miundombinu, madini,
kilimo, na utalii.
Ili kuhakikisha ukuaji huu ni endelevu, serikali imeanza
rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050. Chini ya mkakati wa muda wa kati
(2025–2028), mkazo umewekwa katika: Kuimarisha ukusanyaji wa mapato na
kudhibiti matumizi ya umma mkupitia mifumo ya kidijiti.
Aidha kutokana na mipango mizuri Tanzania ina akiba ya
fedha za kigeni Dola bilioni 6.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa nje
ya nchi kwa zaidi ya miezi mitano.
Diplomasia ya Uchumi: Tanzania Duniani
Kimataifa, Tanzania imeendelea kuimarisha haiba yake
kupitia diplomasia ya uchumi. Rais Samia amesisitiza kuwa ushirikiano wa nchi
katika jumuiya za EAC, SADC, na Umoja wa Mataifa (UN) unalenga moja kwa moja
kuvutia wawekezaji na kukuza biashara.
“Tumetimiza wajibu wetu wa kulinda heshima ya Taifa letu
duniani,” alisema Rais Samia. Aliongeza kuwa serikali itaendelea kutumia
ushirikiano huo kama daraja la kuleta maendeleo ya ndani kwa kuhakikisha
mazingira ya biashara yanabaki kuwa rafiki na yenye kuvutia kwa wawekezaji wa
ndani na nje.
Kwa mtiririko huu wa mafanikio, Tanzania inaingia mwaka
2026 ikiwa na misingi imara ya kiuchumi na kisiasa. Kwa kuunganisha utekelezaji
wa Ilani, Dira ya 2050, na Diplomasia ya Uchumi, Rais Samia anajenga taifa
ambalo si tu ni imara kiuchumi, bali ni mshirika muhimu katika ramani ya
maendeleo ya dunia.

0 Maoni