Katika mkakati kabambe wa kulinda nguvu kazi ya taifa,
Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, imeweka bayana kuwa matumizi ya takwimu
sahihi na uunganishwaji wa fursa ndiyo njia pekee ya kumfanya kijana wa
Kitanzania atulie, aone fursa, na asiyumbishwe na changamoto za sasa na kuwa
bendera hufuata upepo.
Hatua hiyo inafuatia maelekezo ya hivi karibuni ya Waziri
wa Nchi, Mhe. Joel Nanauka, aliyewataka Maofisa Maendeleo ya Vijana nchi nzima
kuwaunganisha vijana na programu za ajira, ujuzi, na uwezeshaji wa kiuchumi.
Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa agizo hili si la
kiutendaji tu, bali ni mhimili wa amani na ustawi wa jamii, kwani moja ya
sababu kuu zinazowafanya vijana kuyumbishwa na kujiingiza kwenye vitendo
visivyofaa ni hisia za kutelekezwa.
Imeelezwa kuwa maofisa maendeleo wanapokuwa na takwimu
sahihi za vijana katika maeneo yao, wanajenga kitu kinachoitwa “Sense of
Belonging”.
"Kijana anapotambuliwa mahali alipo na changamoto zake
kufahamika, anajihisi kuwa sehemu ya mfumo wa nchi. Hii inajenga uzalendo na kumfanya
atulie akijua kuwa serikali inatambua uwepo wake, hali inayopunguza ushawishi
wa makundi yanayoweza kuigawa nchi" anasema Nanauka.
Uchunguzi unaonesha kuwa tatizo si ukosefu wa fursa pekee,
bali ni "Pengo la Taarifa" (Information Gap) ambazo zinawakabili
vijana na hivyo kunatakiwa maofisa hao kuondoa pengo hilo.
" Kuna programu nyingi za kitaifa za ajira na mikopo,
lakini kijana wa kijijini au mtaani mara nyingi hajui pa kuanzia."
alisisitiza.
Kwa kumfanya Ofisa Maendeleo kuwa "daraja" la
moja kwa moja, kijana anaondolewa kwenye hali ya kupapatika. Badala ya kupoteza
muda mitaani, kijana sasa anaelekezwa kwenye programu zenye tija, jambo
linalomsaidia kuweka malengo ya muda mrefu bila kuyumbishwa.
Pia kutokana na Serikali kubaini kuwepo kwa pengo kati ya
mfumo wa elimu na mahitaji ya soko la ajira, maelekezo haya yanalenga kuwapa
vijana ujuzi mpya (Reskilling) unaoendana na soko la sasa.
"Kijana mwenye shughuli inayomwingizia kipato cha
uhakika hawezi kuyumbishwa na ushawishi wa kisiasa au vitendo vya uvunjifu wa
amani," anasema mmoja wa wadau wa maendeleo mkoani Dodoma. Ajira zenye
tija ni kinga dhidi ya chuki na machafuko katika jamii yoyote.
Kwa muda mrefu, baadhi ya mifumo imekuwa ikimtazama kijana
asiye na ajira kama "tatizo" au "kero". Hata hivyo, Katibu
Mkuu, Jenifa Omolo, amesisitiza mabadiliko ya mtazamo. Serikali sasa inamtazama
kijana kama fursa inayohitaji kuendelezwa.
Mtazamo huu mpya unaleta matokeo ya haraka kwa sababu
mipango sasa inaandaliwa kutokana na uhalisia wa takwimu na hoja za vijana
wenyewe (Data-Driven Planning). Hii inaleta matokeo ya kudumu na kurudisha
imani ya vijana kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka
kipaumbele katika kutatua changamoto za kundi hilo.
Wito wa serikali kwa Maofisa Maendeleo ya Vijana ni wito wa
mabadiliko. Ni mkakati unaohakikisha kuwa nguvu, akili, na vipaji vya vijana
vinatumika kujenga nchi badala ya kutumika katika mifarakano. Kwa kutumia
takwimu na uunganishwaji wa fursa, Tanzania inatengeneza kizazi chenye utulivu,
tija, na uzalendo wa dhati.

0 Maoni