Katika salamu za kuaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka
mpya wa 2026, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa taswira ya matumaini kwa
kuanika mafanikio ya Serikali katika kuimarisha uchumi wa taifa.
Licha ya changamoto za kidunia, Tanzania imeweza kudhibiti
mfumuko wa bei, hususan wa bidhaa muhimu za chakula, huku Pato la Taifa likikua
kwa asilimia 5.8. Takwimu hizi si namba tu, bali ni matokeo ya kazi kubwa
iliyofanyika katika sekta za kimkakati kama madini, kilimo, utalii na huduma za
kifedha, jambo linalofanya Deni la Taifa kuendelea kuwa himilivu na endelevu
kwa ajili ya maendeleo ya vizazi vijavyo.
Mafanikio haya ya kiuchumi ni tunda la utulivu ambao nchi
yetu imekuwa nao, na ni lazima tuchukue tahadhari kubwa ili tusiyahujumu kwa
kukosa subira au kurubuniwa na watu wenye nia ovu ya kuchochea mafarakano.
Maoni ya dhihaka yanayoonekana mitandaoni yanayojaribu
kupuuza takwimu hizi za ukuaji ni kielelezo cha uhitaji mkubwa wa ukombozi wa
fikra. Badala ya kubeza jitihada zinazofanyika, ni wakati wa Watanzania
kuungana na kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta za uzalishaji ili
kujikwamua kimaisha. Tukikubali kurubuniwa na sauti za uchochezi zinazotaka
kututoa kwenye mstari, tutaishia kubomoa kile tulichokijenga kwa jasho na damu.
Uzoefu wa matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 unapaswa kubaki
kuwa funzo la kudumu kwetu sote, hususan vijana. Hasira na vurugu siyo njia ya
kutafuta haki, bali ni daraja la kuelekea kwenye uharibifu wa urithi wetu pekee
ambao ni Tanzania.
Ni jukumu la kila kijana kuwa mlinzi wa amani na
mshikamano, akijitenga na makundi yanayopandikiza chuki na kufuata mikumbo
isiyo na tija. Kila hatua tunayochukua kuanzia sasa iwe na lengo la kuijenga
Tanzania tunayotaka kuiona kesho, tukiweka mbele busara na mazungumzo katika
kutatua changamoto zetu badala ya kutafuta visasi au kuingia kwenye mtego wa
taharuki ya kisaikolojia.
Viongozi wa dini na taasisi za kijamii mnao mchango mkubwa
katika safari hii ya kuelekea 2026 kuwa mwaka wa mafanikio na ustawi. Nyie ndio
taa inayopaswa kumulika giza la hofu na kukata tamaa linalojaribu kutandika
mioyo ya wananchi.
Tunawaomba muendelee kuwa daraja la upatanisho na nguzo ya
maridhiano, mkifundisha maadili na kuimarisha welezi wa kiroho miongoni mwa
jamii. Tanzania ni nyumba yetu sote na hatuna nyingine; tuilinde, tuiheshimu,
na tuchangie kuifanya iwe mahali pa amani, utulivu, na ustawi wa kudumu kwa
kila mmoja wetu.

0 Maoni