TMA Yatoa Tahadhari ya Mvua Kubwa Mikoa 20

  

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika mikoa 20 nchini, hali inayoweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwamo mafuriko na maporomoko ya udongo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa leo Desemba 27, 2025, mikoa itakayopata mvua hizo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Tanga, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia. 

TMA imeeleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha kuanzia Jumapili, Desemba 28, 2025, na huenda zikasababisha athari mbalimbali ikiwamo mafuriko, uharibifu wa miundombinu, maporomoko ya udongo pamoja na usumbufu wa shughuli za kiuchumi na kijamii. 

Wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyotajwa, hususan wanaoishi mabondeni na maeneo yenye hatari ya mafuriko, wametakiwa kuchukua tahadhari za mapema ili kulinda maisha na mali zao. 

Aidha, TMA imewasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa mara kwa mara ili kupata taarifa sahihi na za wakati kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Chapisha Maoni

0 Maoni