Tarehe 25 Desemba, 2025, itabaki kwenye kumbukumbu za kihistoria
kama siku ambayo Watanzania walionyesha ukomavu wa hali ya juu na kuiziba mdomo
dunia. Wakati vyombo vya habari vya kimataifa kama CNN, BBC, na majirani zetu
vikiwa vimetega darubini zao vikitabiri vurugu, Watanzania wamejibu kwa Amani,
Upendo, na Utulivu wa kipekee.
Kulikuwa na kampeni kubwa ya uzushi iliyopikwa na watu
wasioitakia mema Tanzania. Walitamani kuona hata mtaa mmoja unawaka moto ili
wapate picha za kuichafua nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa. Lakini, kwa
neema ya Mungu na busara ya watoto wa Nyerere, mipango hiyo imegonga mwamba.
Kuanzia alfajiri ya Krismasi hadi leo, hakuna damu
iliyomwagika, hakuna duka lililoporwa, wala hakuna sintofahamu iliyoripotiwa.
Badala yake, makanisa na maeneo ya starehe yalifurika furaha, huku Watanzania
wakisherehekea kwa umoja.
Baada ya kuona Watanzania wamekataa kuwa "makaa ya
moto," wachochezi kama Mange Kimambi na washirika wake wameibuka na kauli
za hatari na za kukata tamaa. Kwa mara ya kwanza, adui amejionyesha wazi kwa
kuomba nchi yenye nguvu kama Marekani iivamie Tanzania kijeshi.
Hapa ndipo kila mzalendo anapaswa kujiuliza: Hawa watu
wanaitakia nini nchi yetu?Mzalendo haombi nchi yake ipigwe mabomu;Mzalendo
haombi damu ya ndugu zake imwagike;Mzalendo haombi uchumi wa nchi yake
ubomolewe na kwa kuangalia kwa umakini huu unaotangazwa siyo ushindani wa
kisiasa tena; huu ni uhaini na uadui wa wazi dhidi ya Taifa.
Tanzania siyo nchi ya majaribio ya vurugu. Sisi ni kisiwa
cha amani na tutabaki kuwa hivyo. Wale wanaosubiri ripoti za machafuko wataendelea
kusubiri hadi vidole vyao vichoke, maana Watanzania wamechagua Maendeleo mbele,
Amani daima.
"Amani yetu ni tunu, na hakuna chombo cha habari wala
mwanaharakati wa mtandaoni atakayeiweza nguvu ya umoja wa Watanzania."

0 Maoni