Ni dhahiri kuwa kuna mkakati wa makusudi wa kusambaza
taarifa za upotoshaji kuhusu utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam, lakini
uchambuzi wa kina wa kitakwimu na taarifa rasmi za Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA) zinaanika ukweli uliojificha nyuma ya propaganda hizo.
Pamoja na Desemba 14, TPA kutoa taarifa rasmi za kukanusha
madai ya majirani zetu jana taarifa hizo zilirejewa tena mitandaoni ikiwa ni namna ya kusambaza habari za uwongo
mara kadhaa ili ionekane kuwa ya kweli.
TPA tarehe 14 Desemba, 2025, ilikanusha vikali madai ya
mawakala kuelekeza meli katika bandari jirani, ikibainisha kuwa Bandari ya Dar
es Salaam inaendelea kuhudumia idadi kubwa ya meli kwa ufanisi, hususan katika
kipindi hiki cha msimu wa kilele cha mwisho wa mwaka.
Badala ya kusema ukweli yanayojiri katika Bandari ya
Mombasa na kusababisha msongamano uliopo yenyewe ilikuwa ikidai kuwa inatokana
na meli kukimbia Bandari ya Dar es Salaam, kitu ambacho si cha kweli.
Imesemwa kuwa uwepo wa meli nyingi zikisubiri kupakuliwa
bandari ya Mombasa hautokani na ufanisi uliopitiliza, bali ni matokeo ya
mchanganyiko wa msimu wa sikukuu na mgogoro wa kiutawala unaohusu mizigo
iliyokwama katika bandari ya Mombasa.
Msongamano huo unachochewa pakubwa na tozo mpya ya usalama
ya $5,000 kwa kila kontena linaloelekea Sudan Kusini, jambo ambalo
limesababisha mamia ya makontena kukwama gatini na kuziba nafasi kwa meli mpya
zinazotaka kutia nanga. Hali hii ya mizigo iliyokwama (stagnant cargo) ni
tofauti kabisa na ufanisi, na kwa hakika ni "zawadi" kwa Bandari ya
Dar es Salaam kwani wafanyabiashara wa Sudan Kusini sasa wanalazimika kutafuta
njia mbadala zisizo na tozo kandamizi.
Bandari ya Dar es Salaam inayopitia kipindi cha mageuzi
makubwa ya uendeshaji chini ya usimamizi wa DP World, inaendelea kukua kwa
kasi.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa
kwa kuhudumia tani milioni 32.7 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025, huku
shehena za nchi jirani (transit) zikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 29. Hii ni
ishara tosha kuwa Dar es Salaam inachukua takriban asilimia 60 ya mizigo ya
nchi za Kusini kama Zambia, Malawi, na DRC, maeneo ambayo Bandari ya Mombasa
haina ushawishi mkubwa.
Kuhusu muda wa meli kukaa bandarini (vessel turnaround
time), wakati Mombasa inakabiliwa na meli zaidi ya 28 zinazosubiri kutia nanga
kutokana na mkwamo wa miundombinu, Dar es Salaam imeimarisha operesheni za saa
24 na kupunguza muda wa meli kusubiri kupitia mifumo ya kisasa ya TEHAMA na
reli ya SGR.
Licha ya kuwa Mombasa bado inaongoza kwa idadi ya jumla ya
makontena (TEUs) kutokana na uwekezaji wa muda mrefu, Dar es Salaam inakua kwa
kasi kubwa zaidi na inatarajiwa kuvuka makontena milioni 1.1 kufikia mwishoni
mwa mwaka 2025.
Mafanikio haya ya TPA yanathibitishwa na ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotoa hati safi na kuonyesha
faida ya shilingi bilioni 140.48, pamoja na tuzo ya uandaaji bora wa ripoti za
kifedha.
Hivyo basi, simulizi inayojaribu kuipamba Mombasa kama
mshindi wa vita hii ya ufanisi inakosa msingi wa kitakwimu, kwani msongamano wa
majirani zetu ni ishara ya kero za kiutawala na kodi, wakati hali ya Dar es
Salaam ni matokeo ya maboresho ya miundombinu yanayolenga kuiteka Kanda ya
Maziwa Makuu kidijitali na kwa ufanisi wa kudumu.
Pia ukuaji wa bandari unatokana na uendeshaji wa reli ya
SGR ambao unatarajiwa kuwa nguzo kuu ya mabadiliko ya ushindani wa kibiashara
katika Kanda ya Maziwa Makuu kuanzia robo ya kwanza ya mwaka 2026, kwani mfumo
huu unalenga kupunguza gharama na muda wa usafirishaji kwa kiasi kikubwa
kulinganishwa na njia ya barabara inayotumiwa zaidi na Bandari ya Mombasa.
Kwa sasa, Bandari ya Dar es Salaam tayari imeanza kufanya
majaribio ya kusafirisha mizigo kwa reli hiyo kuelekea mikoani na mipakani,
hatua ambayo inatishia moja kwa moja soko la kihistoria la Mombasa nchini
Uganda na Rwanda.
Wakati Mombasa ikikabiliana na changamoto za msongamano wa
meli 28 zilizokwama gatini na tozo mpya za usalama za $5,000 zinazozuia utokaji
wa mizigo, reli ya SGR ya Tanzania inatoa suluhisho la haraka na la uhakika la
kuondoa mizigo bandarini (dwell time) ndani ya siku 4 hadi 7.
Ufanisi huu wa reli utaenda sambamba na uwekezaji wa mifumo
ya kidijitali (paperless clearance) ulioanzishwa na DP World, jambo
litakalopunguza urasimu na kuongeza kasi ya mzunguko wa meli (vessel turnaround
time).
Ikiwa Sudan Kusini na nchi nyingine za kaskazini
zitaendelea kukumbwa na kero za kiutawala na kodi nchini Kenya, reli ya SGR
itatumika kama "zawadi" na kivutio kikuu cha kuhamishia mizigo hiyo
Tanzania, kwani uwezo wa reli hiyo kusafirisha tani nyingi kwa mkupuo mmoja
utapunguza shinikizo la barabarani na kuongeza mapato ya TPA yaliyopangiwa
kufikia shilingi trilioni 1.38. Hali hii itashuhudia Bandari ya Dar es Salaam
ikivuka rekodi yake ya sasa ya kuhudumia tani milioni 32.7 na kujiimarisha kama
lango kuu la biashara linalotumia teknolojia ya kisasa na miundombinu ya
kimkakati kuipiku Mombasa katika soko la kanda.
Kwa maneno mengine hali halisi ya kiuchumi na utendaji wa
bandari nchini Tanzania kwa mwaka 2025 inapingana vikali na madai ya kuwepo kwa
msongamano nchini Kenya kutokana na mzigo unaohamishwa kutoka Bandari ya Dar es
Salaam.
Ukweli ni kwamba Bandari ya Dar es Salaam imehitimisha
mwaka wa fedha 2024/25 kwa rekodi ya kihistoria, ikishughulikia shehena ya
mizigo iliyofikia tani milioni 32.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kutoka
tani milioni 23.69 za mwaka uliopita.
Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji
wa kimkakati wa wabia kama DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal,
ambao wameongeza ufanisi wa operesheni na kukuza mapato ya Serikali.
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) sasa ni kinara katika
kutoa gawio la asilimia 15 ya mapato ghafi kwa Serikali, ikitoa shilingi
bilioni 181.5 mwaka 2025 ikilinganishwa na shilingi bilioni 153.917 mwaka 2024.
Maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es
Salaam yamepunguza muda wa wafanyabiashara kusubiri na kupokea mizigo yao
kutoka siku kumi hadi kufikia siku tatu pekee.
Ufanisi huu umeongeza imani ya wadau wa usafirishaji,
ambapo meli kubwa za kisasa kama Grande Shanghai, zenye uwezo wa kubeba magari
9,000 kwa wakati mmoja, zimeanza kutia nanga nchini kutokana na upanuzi wa
miundombinu na mifumo imara ya huduma.
Kwa sasa, mapato ya bandari yamefikia wastani wa shilingi
trilioni moja kwa mwezi, jambo linaloashiria kuwa Bandari ya Dar es Salaam
haijapoteza mwelekeo bali imezidi kuimarika kama kitovu kikuu cha biashara
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande mwingine, msongamano unaoshuhudiwa katika
Bandari ya Mombasa unatokana na migogoro ya kodi na mkwamo wa miundombinu ya
ndani na si kwa sababu ya "kuiba" soko la Tanzania. Kitendo cha
mamlaka za Kenya kutoza ada ya usalama ya dola 5,000 kwa kila kontena
linaloelekea Sudan Kusini kimesababisha mamia ya makontena kukwama gati na
kuzuia nafasi kwa meli nyingine.
Msongamano huu wa meli 28 zinazosubiri Mombasa ni ishara ya
ucheleweshaji wa huduma (vessel turnaround time), wakati Dar es Salaam
imefanikiwa kuondoa mkwamo huo kupitia mifumo ya kidijitali na operesheni za
saa 24. Hivyo, wakati Mombasa ikikabiliana na malalamiko ya Sudan Kusini na
kero za kodi, Dar es Salaam inazidi kuimarika kama kitovu cha uhakika cha
biashara kwa nchi za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Kukwama kwa mamia ya makontena bandarini na kuwafanya
mawakala wa usafirishaji kuepuka mizigo inayoelekezwa Juba, hivyo kuongeza
msongamano usio wa lazima umesesababisha
Sudan Kusini kuanza kutafuta njia mbadala, ikiwemo ujenzi wa kituo
katika Bandari ya Djibouti ili kupunguza utegemezi kwa Bandari ya Mombasa.
Wakati Mombasa ikikabiliwa na mkwamo huu wa kodi na
msongamano wa meli zinazosubiri gati, Bandari ya Dar es Salaam inaendelea
kupokea shehena kubwa ya mizigo ya transit, huku nchi jirani zikizidi kutumia
bandari hiyo kutokana na mazingira rafiki ya kibiashara na mifumo ya kisasa ya
ulinzi wa mizigo.
Ukweli ni kwamba madai yanayoenezwa kuhusu kuhamishwa kwa
mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Mombasa hayana msingi wa
kitakwimu, bali yanachangiwa na msimu wa kilele wa mahitaji ya mwisho wa mwaka.
Ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeimarika kwa kiwango
kikubwa ambapo muda wa meli kukaa bandarini umepungua kutoka siku kumi hadi
kufikia siku tatu pekee, huku mapato yakiongezeka na kufikia wastani wa
shilingi trilioni moja kwa mwezi.

0 Maoni