Hali ya amani na utulivu iliyoshuhudiwa jijini Dar es
Salaam katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka wa 2025 ni kielelezo
tosha cha utashi wa Watanzania kulinda mshikamano wa kitaifa dhidi ya mivutano
ya kisiasa.
Maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi katika
maeneo mbalimbali ya burudani wakisherehekea Krismasi na siku ya kupeana zawadi
ya Boxing Day, huku kukiwa na mazingira ya usalama wa hali ya juu
yaliyowezeshwa na uratibu makini wa vyombo vya dola.
Katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama Fukwe za
Coco na kituo cha biashara cha Mlimani City, uwepo wa jeshi la polisi linalofanya
doria kwa miguu, farasi, na magari umetoa uhakika wa usalama kwa kila familia
iliyojitokeza kufurahia mapumziko hayo.
Utulivu huu una thamani ya kipekee ukizingatia kuwa
unatokeo wakati kukiwa na jaribio la baadhi ya wanaharakati kuhamasisha maandamano
katika kipindi hiki cha sikukuu, baada ya kushindwa kwa mipango yao ya awali ya
maandamano haramu ya tarehe 9 Desemba, 2025.
Hata hivyo, Watanzania wameonyesha ukomavu mkubwa kwa
kukataa shinikizo hizo na badala yake kuitikia wito wa kulinda amani, wakitambua
kuwa ustawi wa uchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja unategemea utengamano wa
nchi. Hatua hii ya wananchi kuipongeza serikali na polisi inaakisi imani kubwa
ya umma katika usimamizi wa usalama unaoruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi
kuendelea bila hofu.
Amani hii inayotawala mitaani inaenda sambamba na utulivu
siyo tu inaimarisha furaha ya sikukuu, bali pia inatoa taswira chanya kwa
wawekezaji na wadau wa biashara kuwa Tanzania inasalia kuwa kisiwa cha amani na
mhimili wa uchumi wa kanda.
Uamuzi wa Watanzania kulinda amani kinyume na harakati za
vurugu umesaidia kudumisha mazingira bora ya biashara na huduma, ambapo hakuna
malalamiko yoyote ya uchelewaji au usumbufu yaliyoripotiwa katika kanda nzima
ya biashara. Hii inathibitisha kuwa nguvu ya umma imejielekeza katika kulinda
mustakabali wa Taifa na ustawi wa kila mwananchi, ikizika rasmi ajenda za
uchochezi na kuifanya Boxing Day ya mwaka 2025 kuwa alama ya amani ya kudumu
nchini Tanzania.

0 Maoni