Wakati dunia ikishuhudia mataifa kadhaa yakisambaratika
kutokana na unyakuzi wa madaraka na machafuko ya kijamii, Tanzania imezidi
kung’ara kama kisiwa cha utulivu, hali inayochagizwa na uelewa wa wananchi wake
kuhusu thamani ya amani.
Kauli ya Sheikh Hilal Shawej, maarufu kama Sheikh Kipozeo,
aliyoitoa Desemba 25, 2025, imekuja wakati muafaka kuwakumbusha Watanzania kuwa
bila amani, hakuna jukwaa la kudai haki. Sheikh Kipozeo amewanyooshea vidole
baadhi ya viongozi wa dini na wanaharakati wanaojaribu kupandikiza hoja kuwa
haki ni bora kuliko amani, akibainisha kuwa msimamo huo ni hatari na unaweza
kulifikisha Taifa katika lindi la vurugu.
Tofauti na nchi kama Libya, Sudan, DRC, na Syria, ambako
mamilioni ya watu wamepoteza maisha na wengine kuwa wakimbizi kwa kisingizio
cha kupigania haki, Tanzania imeweza kudumisha mifumo yake ya kisheria na
kijamii kufanya kazi kwa sababu ya utulivu uliopo.
Katika kile kinachoonekana kama kujibu hoja za
viongozi wa Kikristo wanaotaka haki
kwanza , Sheikh Kipozeo amehoji ni mazingira gani yataruhusu madai ya haki
kufanikiwa ikiwa amani itatoweka na kila kitu kuvurugika. Amesema kuwa amani
ndiyo nguzo kuu inayowezesha taasisi, mifumo ya kisheria, na jamii kwa ujumla
kufanya kazi, hivyo bila utulivu huo hata hiyo haki inayodaiwa haiwezi
kufikiwa.
“Ukisema haki ni bora kuliko amani, unatatanisha kidogo,
kwa sababu hiyo haki utaipata vipi bila ya amani kwanza? Haki haiwezi
kupatikana bila ya amani. Amani na utulivu ndiyo kila kitu, bila amani kila
kitu kinavurugika,” amesisitiza Sheikh Kipozeo katika maelezo yake yaliyojaa
busara.
Sheikh Kipozeo amehoji kwa uchungu: “...hiyo haki utaipata
vipi bila ya amani kwanza?”. Hali ya nchi hizo zilizotajwa ni ushahidi mchungu
kuwa, mara tu amani inapotoweka, hata haki ya kuishi, haki ya kupata chakula,
na haki ya kuabudu hupotea na kubaki kuwa ndoto.
Sheikh Kipozeo amewataka Watanzania kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kuijalia nchi kuendelea kuwa na usalama, akisisitiza kuwa amani ndiyo
chachu ya maendeleo na ustawi wa Taifa.
Aidha, amewakumbusha waumini wajibu wao wa kidini wa
kukataza maovu na kuamrisha mema kama misingi mikuu ya kudumisha utulivu huo.
Sheikh Kipozeo amewakumbusha Watanzania wajibu wa kukataza
maovu na kuamrisha mema kama njia ya kuitunza tunu hii ya amani. Maendeleo
makubwa ya kiuchumi yanayoshuhudiwa nchini, ikiwemo ufanisi wa miradi ya
kimkakati, ni matokeo ya moja kwa moja ya utulivu huu ambao sasa unapaswa
kulindwa dhidi ya hoja zenye mwelekeo wa kutaka kuvuruga mshikamano wa kitaifa.
Ukomavu huu wa amani umeonekana wazi katika jiji la Dar es
Salaam wakati wa sherehe za Boxing Day. Licha ya kuwepo kwa uchochezi na hamasa
za vurugu kutoka kwa baadhi ya wanaharakati waliokuwa wakishinikiza maandamano
haramu baada ya mipango yao ya Desemba 09, 2025 kushindwa, wananchi wamekataa
kuitikia wito huo.
Badala yake, maelfu wamejitokeza katika fukwe za Coco na
Mlimani City, wakionyesha kuwa wanatambua umuhimu wa amani kwa mustakabali wa
maendeleo yao na ustawi wa Taifa.

0 Maoni