Wakati mataifa jirani yakitapatapa kurejea katika hali ya
kawaida ya kitalii huku yakikumbwa na migogoro ya kisiasa na mdororo wa
kiuchumi, Tanzania imepiga hatua ya kihistoria ambayo sasa imeibua "wivu
wa kibiashara" na kampeni za chini kwa chini za kujaribu kuichafua nchi.
Serikali imejibu mapigo kwa takwimu nzito zinazothibitisha
kuwa Tanzania si tu ni kisiwa cha amani, bali ndiyo kiongozi wa utalii katika
ukanda wa Afrika Mashariki, jambo ambalo limekuwa mwiba kwa washindani
wanaotumia vyombo vya habari vya nje kupika habari za uongo.
Ukuaji wa Kishindo: Takwimu Hazidanganyi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan
Abbas, amebainisha kuwa kati ya Januari na Novemba 2025, Tanzania imerekodi
ongezeko la asilimia 9 ya watalii wa kimataifa. Hili ni ongezeko la watalii 173,000
ndani ya miezi 11 pekee idadi ambayo ni sawa na jumla ya watalii wanaoingia
katika baadhi ya nchi jirani kwa mwaka mzima.
Wakati majirani wakisuasua kwa ukuaji wa asilimia 3 hadi 5,
kasi ya Tanzania imeiacha kanda hiyo gizani, ikichukua kipande kikubwa cha
"keki ya utalii" barani Afrika.
Amani ya Tanzania: Bidhaa Isiyoweza Kununuliwa
Siri ya mafanikio haya imetajwa kuwa ni amani na utulivu wa
kipekee wa Kitanzania. Dkt. Abbas amefafanua kuwa wakati baadhi ya nchi washindani
zikikumbwa na maandamano ya mara kwa mara na hali ya sintofahamu, Tanzania
imebaki kuwa kimbilio salama.
Hali hii ndiyo inayowasukuma "wachawi wa utalii"
kutengeneza picha za uongo mitandaoni wakidai nchi haina usalama. Hata hivyo,
ukweli ni kwamba hoteli nyingi nchini sasa zimejaa (fully booked) hadi mwanzoni
mwa mwaka 2026, jambo linaloziba vinywa vya wale wanaodai "beach hakuna
hata wa dawa."
Mapinduzi ya TAWA: Utalii wa Ndani kama Kinga
Katika hatua ya kimkakati ya kujenga "jeshi la
ndani" la kulinda utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA)
imeleta wanyama wakali na wa ajabu kama simba, tembo, na duma katikati ya jiji
la Dar es Salaam katika Viwanja vya Sabasaba.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TAWA, Mlage Kabange, amesema
maonyesho hayo (Desemba 20 - Januari 5) yanalenga kumfanya kila Mtanzania kuwa
balozi wa rasilimali zake. Kwa kiingilio rafiki cha Sh. 4,000, Serikali
inatengeneza ukuta imara dhidi ya kuyumba kwa soko la kimataifa, ikihakikisha
kuwa utalii unakuwa sehemu ya maisha ya mwananchi.
Jibu kwa Propaganda za Nje
Serikali imesisitiza kuwa juhudi za "kumchafua
jirani" ili kupora wageni zimeshindwa mbele ya ukweli wa takwimu na
miundombinu imara iliyochochewa na miradi kama The Royal Tour. Viwanja vya
ndege vya Tanzania vinaendelea kupokea ndege kubwa za kimataifa kila siku, huku
watalii wakimiminika kushuhudia maajabu ya nchi hii.
Ujumbe wa Serikali:
"Tanzania ni kielelezo, na mafanikio yetu ndiyo
yanayowaumiza wanaotutakia vurugu. Tutaendelea kupambana na propaganda kwa
kutumia ukweli, kulinda rasilimali zetu, na kuwakaribisha wageni kwa upendo
uleule wa Kitanzania," alisisitiza Dkt. Abbas.

0 Maoni